Viongozi wa dini ya Kikristo, wasomi na wanasiasa wamewakosoa waandaaji wa hafla ya ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki iliyoandaliwa na mji mkuu wa Ufaransa, Paris, kutokana na onyesho la “Drag Queens” la mwanamume aliyevaa mavazi ya kike na kujikwatua na taswira ya mchoro wa “Karamu ya Mwisho,” (Last Supper) ambayo baadhi wanasema inaonyesha picha ya Nabii Isa, amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake, na wanafunzi wake.
Hayo yalishuhudiwa katika hafla ya ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki ya Paris 2024 Ijumaa wiki hii ambayo utaendelea hadi tarehe 11 mwezi ujao wa Agosti.
Tofauti na hafla za miaka ya iliyopita, walioshiriki waliingia kwenye hafla ya Michezo ya Olimpiki wakiwa kwenye boti 85 zilizovuka Mto Seine, katika tukio hilo linaloshirikisha wanariadha kutoka nchi 205.
Baadhi ya vipengele vya maonyesho ya ufunguzi huo vimekosolewa vikali, vikitajwa kuwa ni kampeni ya imani za kishetani na kueneza ushoga, haswa kipengee cha tamthilia ya picha ya “Karamu ya Mwisho” ya Leonardo da Vinci, kupitia wahusika waliobadilisha jinsia (Drag Queens), ambayo wakosoaji wanasema kuwa ni tusi la kimakusudi kwa Ukristo na dini za Mwenyezi Mungu.
Katika hafla hiyo ya Michezo ya Olimpiki Paris 2024, nafasi ya “Kristo” katika uchoraji wa Karamu ya Mwisho, aliwekwa mtu aliyekuwa uchi, ambaye wakosoaji wanasema kwamba aliwakilisha Dionysus, mungu wa divai ambaye pia alijulikana kwa desturi zake za kipagani na zisizo na maadili.
Jana Jumamosi, maaskofu wa Ufaransa walichapisha maoni yao kuhusu sherehe ya ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki ambayo sehemu yake moja imesema: “Inasikitisha kwamba tamasha hili lilikuwa na matukio yanayodhihaki Ukristo, na tunakabiliana na hali hii kwa huzuni kubwa.”
Taarifa ya maaskofu wa Ufaransa iliwashukuru wafuasi wa dini nyingine kwa kuonyesha mshikamano wao na Wakristo katika kukabiliana na hali hiyo.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban ameshambulia vikali hafla ya ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki Paris 2024 akikosoa “udhaifu na mporomoko wa kimaadili wa nchi za Magharibi.”
Waziri Mkuu wa Hungary amesema kuwa sherehe hiyo, ambayo ilifanyika Ijumaa kwenye Mto Seine, ni kielelezo cha “utovu” wa kimaadili katika nchi za Magharibi na kuongeza kuwa: “Wamagharibi wanaachana taratibu na uhusiaino wa kiroho na kifikra na Muumba, nchi na familia, jambo ambalo limesababisha kuzorota kwa maadili ya umma katika jamii, kama tulivyoona katika sherehe za ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki siku ya Ijumaa.”
Katika muktadha huo, kasisi wa Kanisa Katoliki la Kirumi huko Ramallah, Abdullah July, amelaani kitendo cha Ufaransa cha kuwatumia mashoga katika sherehe za ufunguzi wa Olimpiki kuwakilisha sura ya ‘Yesu Kristo’, akitaja suala hilo kuwa ni “hatari kubwa.”
Kasisi July amesema: “Hairuhusiwi kumwakilisha Yesu Kristo kwa njia hii ambayo inakiuka mambo matakatifu na kwamba huo ni mchakato wa kimakusudi wa kupotosha dhana ya dini na kupiga vita dini kwa ujumla, sio tu dini ya Kikristo.”