Haki za binadamu ya Yemen: Saudia imeua makumi ya wahajiri wa Kiafrika

Kaimu Waziri wa Haki za Binadamu wa Yemen amelaani mauaji ya wahajiri wa Kiafrika yaliyofanywa na walinzi wa mpaka wa Saudi Arabia.

Mtandao wa Al-Masira nchini Yemen umepata picha zinazoonyesha kwamba, walinzi wa mpaka wa Saudi Arabia waliwaua makumi ya wahajiri wa Kiafrika kwenye mpaka wa nchi hiyo na Yemen.

Ripoti hiyo imesema, Waafrika walionusurika katika mauaji hayo wamethibitisha kuwa wanajeshi wa Saudia waliwaua kwa makusudi makumi ya wahajiri wa Ethiopia kwa kutumia umeme baada ya kuwakusanya katika chumba kimoja.

Kwa mujibu wa mtandao wa habari wa al-Masira, “Ali al-Dilami” amesema, Wizara ya Haki za Binadamu ya Yemen imelifahamisha Shirika la Kimataifa la Wahajiri kuhusu mauaji ya wahajiri wa Kiafrika kwenye mpaka wa Yemen na Saudi Arabia, lakini inasikitisha kuona kwamba, jamii ya kimataifa haijachukua hatua yoyote kuhusu hali mbaya inayowakabili wahanga hao.

Al-Dilami amesisitiza kuwa Wizara ya Haki za Binadamu ya Yemen iko tayari kutoa nyakati muhimu kwa upande wa Ethiopia ili kuthibitisha jinsi Saudi Arabia ilivyokiuka Sheria ya Kimataifa ya Wakimbizi na Mkataba wa 1951 wa Hali ya Wakimbizi, na ameitaka Ethiopia kuokoa maisha ya wahamiaji wengine wa Kiethiopia na kulaani jinai za Saudi Arabia dhidi ya wahajiri hao.

Kaimu Waziri wa Haki za Binadamu wa Yemen pia ameitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua kukomesha maafa hayo.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *