Nikki Haley mwenye azma ya kuteuliwa na chama cha Republican kuwa mgombea wake wa urais katika ujao nchini Marekani ametoa matamshi ya kujikanyaga akidai kuwa, njia pekee ya kukomesha vita vya Ukraine ni kuendelea mapigano baina ya Russia na Ukraine, na eti kushindwa Kiev katika vita hivyo kutaibua Vita vya Tatu vya Dunia.
Haley ambaye ni Mwakilishi wa zamani wa Marekani katika Umoja wa Mataifa amesema lengo la Washington kuendelea kuipa Ukraine silaha ni kukomesha vita baina ya nchi hiyo na Russia, sambamba na kutuma ujumbe mzito kwa mahasimu wa Marekani.
Haley ambaye pia amewahi kuwa Gavana wa South Carolina ameeleza kuwa, kushinda Ukraine katika vita hivyo ni kwa maslahi ya Marekani.
Amedai kwamba, “Kushinda Ukraine kutatuma ujumbe kwa China juu ya Taiwan, ujumbe kwa Iran inayotaka kuunda bomu, ujumbe kwa Korea Kaskazini inayofanyia majaribio makombora ya balestiki na ujumbe kwa Russia kwamba imesambaratika.”
Hivi karibuni, Dmitry Medvedev, Naibu wa Mkuu wa Baraza la Usalama la Russia alisema kwamba mabwana na viongozi wa Magharibi ndio wanaowaamulia viongozi vya Kiev nini cha kufanya.
Rais wa Russia Vladimir Putin, mnamo Februari 24, 2022 alianzisha oparesheni za kijeshi nchini Ukraine akiwa anaitikia ombi la msaada wa kijeshi kutoka kwa wakuu wa mikoa ya Donetsk na Luhansk mashariki mwa Ukraine ambao walitajangaza kujitenga maeneo hayo.
Tangu kuanza kwa vita hivyo, Marekani na washirika wake wa Magharibi wamekuwa wakiipatia Kiev zana za kijeshi zenye thamani ya makumi ya mabilioni ya dola. Silaha zilizotolewa ni pamoja na mifumo ya roketi, ndege zisizo na rubani, vifaru na magari ya kivita na mifumo ya mawasiliano.