Hali mbaya ya wanawake nchini Ufaransa; kielelezo cha unyanyasaji wa wanawake katika nchi za Magharibi

Licha ya kuwa nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani siku zote zimekuwa zikidai kutetea haki za binadamu zikiwemo haki za wanawake, lakini tunapotazama takwimu na ripoti za vyombo vya habari katika uwanja huu tunakutana na taswira ya kutisha ya hali mbaya ya wanawake katika jamii za nchi za Magharibi.

Ufaransa ambayo ni miongoni mwa nchi vinara wa uliberali wa Kimagharibi, ina hali mbaya katika uga wa wanawake na haki zao. Kulingana na ripoti iliyochapishwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ufaransa kuhusu takwimu za mauaji ya wanawake mwaka uliopita wa 2021, idadi ya wanawake waliouawa na waume zao imeongezeka kwa asilimia 20 nchini humo. Kwa mujibu wa data zilizotolewa kwenye ripoti hiyo iliyochapishwa chini ya kichwa cha maneno: “Mauaji ya Kikatili Kati ya Wanandoa”, mnamo 2021 wanawake 122 waliuawa na waume zao wa sasa au wa zamani. Kwa utaratibu huo, kwa wastani, mwaka jana kulishuhudiwa mauaji ya mwanandoa mmoja  nchini Ufaransa kila baada ya siku mbili na nusu. Kama ilivyokuwa miaka ya nyuma, wanawake ndio wahanga wakuu wa mauaji ya ndani ya familia. Mwaka 2020, wanawake 102 na mwaka 2019 wanawake 146 waliuawa katika ukatili ulioshuhudiwa kati ya wanandoa huko Ufaransa. Kati ya 2020 na 2021, unyanyasaji wa majumbani nchini Ufaransa uliongezeka kwa asilimia 21, na sehemu kubwa ya ukatili huo ulikuwa wa kimwili. Kesi 208,000 za unyanyasaji wa wajumbani zilizosajiliwa mwaka huu wa 2022 ziliwasilishwa kwenye vyombo husika au taasisi za usalama.

Suala jingine linalotia wasiwasi katika jamii ya Ufaransa ni kiwango cha juu cha unyanyasaji wa kijinsia katika sehemu za kazi. Kulingana na utafiti wa Taasisi ya Kutetea Haki za Binadamu iliyochapishwa mwaka 2015, mwanamke mmoja kati ya kila watano amekuwa mwathirika wa unyanyasaji wa kijinsia maeneo ya kazi. Nchini Ufaransa, wanawake ndio waathiriwa wakuu wa unyanyasaji wa kijinsia na wanasumbuliwa na tatizo hilo katika nyanja zote za maisha yao, ikiwa ni pamoja na ndani ya familia, kwenye maisha ya ndoa, mahali pa kazi na maeneo ya umma. Ripoti iliyochapishwa na Taasisi ya Taifa ya Takwimu ya Ufaransa mwaka 2016 ilionesha kuwa, ukatili wa kingono huathiri wanawake 600,000 nchini Ufaransa kila mwaka. Hapana shaka yoyote kwamba hivi sasa takwimu hizi zimeongezeka sana ikilinganishwa na mwaka huo wa 2016.

Hali mbaya na ya kutisha ya wanawake nchini Ufaransa imelifanya suala la kutetea haki za wanawake na kukabiliana na ukatili dhidi yao kuwa kadhia muhimu katika uga wa kisiasa wa nchi hiyo ya Ulaya.

Kimsingi, tunapoangalia hali ya wanawake katika nchi za Magharibi zinazodai kutetea haki zao tunaona kuwa wanawake katika nchi hizo wanakabiliwa na hali mbaya, na haki zao za kibinadamu zinapuuzwa. Ubaguzi dhidi ya wanawake, hasa katika masuala ya ajira na haki za kijamii upo wazi, na kuna ukosefu mkubwa wa usawa kati ya wanawake na wanaume katika suala la mishahara na ajira katika nchi kama vile Marekani, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Canada. Vilevile, wanawake wanatambuliwa kuwa ndio waathirika wakuu wa unyanyasaji wa kijinsia na ukatili wa kimwili katika nchi za Magharibi, na takwimu zinazotolewa katika uwanja huu zinaonyesha wazi suala hili. Wanawake wanachukuliwa kuwa ni binadamu wa daraja la pili katika nchi za Magharibi na hawana usalama unaohitajika wala hawapewi himaya ya dhati na serikali za Magharibi; kinyume chake wanatambuliwa kama nyenzo za kushibisha hamu na matakwa ya wanaume.

Kwa mujibu wa utafiti wa Reuters, Marekani inahesabiwa kuwa ni kati ya nchi 10 zisizo salama kwa wanawake; nafasi ambayo imekuwa nayo bila kubadilika kwa angalau muongo mmoja uliopita. Kwa hakika, moja kati ya vielelezo muhimu vya kuporomoka kimaadili mfumo wa ustaarabu wa Kimagharibi ni suala hili la ukandamizaji na ubaguzi dhidi ya wanawake, na mamilioni ya wanawake katika nchi za Magharibi wanakabiliwa na unyanyasaji wa nyumbani.

Utumiaji wa wanawake kama chombo katika maswala ya utangazaji, tishio kwa taasisi ya familia, kuenea kwa aina mbalimbali za ufuska na ukandamizaji na ukatili wa kingono dhidi ya wanawake kwa kutumia jina la uhuru, mishahara isiyo sawa katika hali na mazingira sawa ya kazi bila kujali uwezo wa kimwili na kiroho wa wanawake, mazingira yasizo salama ya kazi na elimu, takwimu za kutisha za unyanyasaji na ubakaji wa wanawake katika maeneo ya kazi na shuleni, ubaguzi wa rangi, ongezeko la idadi ya wafungwa wa kike na ukati dhidi yao, kiwango kikubwa cha utoaji mimba, umaskini, kuenea kwa ukahaba na magendo ya wanawake, ni miongoni mwa madhihirisho ya kupuuzwa haki za wanawake katika nchi za Magharibi.

Maryam Mahmoudzadeh, profesa wa chuo kikuu na mtaalamu wa masuala ya wanawake, anasema: “Licha ya kukiri kwa vyombo vya habari na ripoti nyingi kutoka nchi za Magharibi kuhusu unyanyasaji na ukatili unaofanyika dhidi ya wanawake, bado nchi hizo zinajiona kuwa watetezi wa haki za binadamu. Unyanyasaji mkubwa zaidi dhidi ya wanawake duniani unaripotiwa katika nchi za Uingereza, Marekani na Ufaransa, lakini bado nchi hizo zinadai kuwa vinara wa haki za binadamu.”

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *