Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) katika mji wa Quds amesema kuwa, serikali mpya ya utawala wa Kizayuni wa Israel inayoongozwa na Benjamin Netanyahu inadhihirisha sura ya watenda jinai na kusisitiza kuwa: Adui haelewi isipokuwa lugha ya mabavu.
Mohammed Hamada amesema msimamo wa Hamas mkabala wa utawala wa Kizayuni unaotenda jinai ni kwamba utawala huo haufahamu chochote isipokuwa lugha ya mapambano. Hamada ameeleza kuwa, serikali ya mrengo wa kulia na yenye misimamo mikali ya Israel imefichua sura halisi ya watenda jinai wa utawala huo.
Msemaji wa Hamas huko Quds ameongeza kuwa, msimamo wa harakati hiyo ya mapambano ya Kiislamu mkabala wa serikali mpya na serikali yoyote itakayochukkua madaraka huko Israel ni kwamba, lugha ya mabavu na muqawama pekee ndio itakayokuwa jibu kwa serikali hiyo.
Hamada ameongeza kuwa, Vita vya Upanga wa Quds viliziunganisha pamoja harakati na makundi yote kwa ajili ya kuulinda Msikiti wa al Aqsa na kwamba, upanga huo hautawekwa chini hadi hapo Maghasibu wa Kizayuni watakapofukuzwa huko Quds, na Msikiti wa al Aqsa utakapokombolewa.