Afisa mwandamizi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS amekosoa sera za kuuma na kupuliza za jamii ya kimataifa kuhusiana na jinai za kila siku zinazofanywa na Wazayuni dhidi ya Msikiti mtukufu wa Al-Aqsa.
Khalil al-Hayya, mkuu wa kitengo cha mahusiano na nchi za Kiarabu na Kiislamu katika harakati ya Hamas amebainisha ukosoaji huo katika mkutano na Mratibu maalumu wa Umoja wa Mataifa katika mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati Tor Wennesland.
Katika mazungumzo yaliyofanyika Ukanda wa Gaza kati ya mjumbe huyo maalum wa Umoja wa Mataifa na ujumbe wa Hamas ukiongozwa na al-Hayya, pande hizo mbili zimejadiliana na kubadilishana mawazo kuhusu athari hatarishi zinazowakabili Wapalestina, mji wa Baitul Muqaddas na Msikiti wa Al-Aqsa kutokana na baraza jipya la mawaziri litakaloundwa na utawala wa Kizayuni pamoja na mipango ya kibaguzi na kifashisti iliyoratibiwa na baraza hilo.
Katika kikao hicho, ujumbe wa Hamas umesisitiza juu ya haki ya wananchi na vyama vya Palestina kuonyesha muqawama wa kukabiliana na utawala ghasibu wa Kizayuni na kutahadharisha kuwa, sera na vitendo vya kichochezi vinavyofanywa katika mji wa Quds na katika Msikiti wa Al-Aqsa vitaifanya hali ya mambo isiweze tena kudhibitika.
Ujumbe huo wa Hamas umesisitiza pia kuwa, Ukanda wa Gaza na watu wake ni sehemu ya ardhi kubwa ya Palestina, na wanafuatilia kwa uchungu mkubwa matukio ya maeneo yote ya Palestina hususan Baitul-Muqaddas, Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan unaokaliwa kwa mabavu na ardhi zilizoanza kukaliwa kwa mabavu mwaka 1948, na licha ya mzingiro na uchokozi mtawalia inaofanyiwa Ukanda wa Gaza, hawataacha kutoa mchango wao wa kihistoria wa kuwaunga mkono Wapalestina popote pale walipo.
Ujumbe huo wa harakati ya Hamas umeitaka jamii ya kimataifa kupitia mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa uachane na sera ya kuuma na kupuliza na kuchukua hatua za kivitendo ili kuzima hujuma za Wazayuni dhidi ya wananchi wa Palestina na maeneo yao matakatifu.
Takriban kila siku, msikiti wa Al-Aqsa unashuhudia mashambulizi makubwa ya walowezi wa Kizayuni, wanaoingia kwa wingi msikitini humo wakiungwa mkono na jeshi la utawala wa Kizayuni.