Hamas: Jinai za utawala wa Kizayuni hazitawatia hofu watu wa Wapalestina

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imetoa taarifa ikiilaani jinai za Wazayuni huko Jenin na kusisitiza kuwa: Jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel na mauaji yake dhidi ya raia wa Palestina kamwe hazitalitia hofu taifa hilo.

Ni baada ya wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel kushambulia mji wa Jenin katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan jana Jumanne na kuua Wapalestina wasiopungua 6.

Harakati ya Hamas imewataka wananchi wa Palestina kuwa na msimamo thabiti katika kukabiliana na utawala ghasibu wa Israel na jinai zake, kulipiza kisasi cha damu ya mashahidi wa Jenin na kushikamana barabara na wasio wa mashahidi kuhusiana na kujitolea na kudumisha mapambano kama njia pekee ya kuikomboa Palestina na kuwarejesha nchini wakimbizi wa Kipalestina.

Hamas pia imewataka wananchi wa Palestina kuendelea kuwa macho na kuwalenga askari na walowezi wa Kizayuni kila mahali katika ardhi inayokaliwa kwa mabavu ya Palestina.

Idadi kubwa ya askari wa kikosi maalumu cha jeshi la utawala haramu wa Israel ilivamia mji wa Jenin na kambi za wakimbizi na kukabiliwa na mapambano makali wanamapambano wa Kipalestina. Hujuma hiyo imefanyika sambamba na mashambulizi mengine ya jeshi la Israel katika mji wa Nablus.

Ofisi ya Rais wa Palestina imesema kuwa, mauaji ya kila siku yanayofanywa na askari wa utawala ghasibu wa Israel  ni vita vya pande zote na jitihada za kuharibu juhudi za kurejesha utulivu.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina pia imetoa taarifa ikisema kwamba mauaji na mashambulizi ya Israel huko Jenin na Nablus ni uthibitisho kwamba utawala huo ghasibu umechagua njia ya kukuzidisha mivutano.

Sambamba na hayo operesheni za kukabiliana na jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika maeneo mbalimbali ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, zimeongezeka sana katika miezi ya hivi karibuni; kwa kadiri kwamba baadhi ya viongozi wa kisiasa na taasisi za kijeshi na usalama za utawala huo zinakiri kwamba zinaelemewa kukabiliana na operesheni hizo na kuonya kuhusu kupanuka kwake.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *