Kiongozi mmoja mwandamizi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema kuwa, jukumu kuu la kambi ya muqawama ni kuhakikisha ardhi zote za Palestina zinakombolewa na hiyo maana yake ni kufutwa katika uso wa dunia, utawala pandikizi wa Kizayuni ambao unazikalia kwa mabavu ardhi za Palestina.
Shirika la habari la FARS limemnukuu Mahmoud al Zahar, mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya HAMAS akisema hayo kwenye kipindi cha al Mihwar kilichoendeshwa na “Radio Alaqsa” na ameishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa msaada wake mkubwa kwa muqawama na mapambano ya ukombozi ya wananchi wa Palestina.
Al Zahar ameiambia Radio Alaqsa kwamba, mapambano ya “Wa’dul Aakhirah” (jina ambalo HAMAS imeyapa mapambano ya mwisho ya kukombolewa kila shibri ya ardhi ya Palestina), yamekaribia sana na inabidi tujiandae kwa mapambano hayo.
Amesema, Baytul Muqaddas au Quds, si tu ni mji mkuu wa Palestina unaokaliwa kwa mabavu na Wazayuni, lakini pia ni sehemu ya itikadi ya Kiislamu, na ni kiunganishi cha Misikiti Miwili Mikuu, Masjidul Aqsa na Masjidul Haram; mmoja ni Kibla cha Kwanza na mwingine ni Kibla cha hivi sasa cha Waislamu wote.
Kiongozi huyo wa ngazi za juu wa HAMAS pia amegusia mapambano ya harakati za Palestina katika Ukingo wa Magharibi na kusema: “Harakati za muqawama na mapambano katika Ukingo wa Magharibi zimepelekea utawala wa Kizayuni wa Israel uingiwe na kiwewe na uchanganyikiwe kwani hali katika eneo hilo ni sawa na ya mapambano ya Ukanda wa Gaza.” Amesema hivi sasa kunashuhudiwa Wapalestina wakiuawa shahidi kila leo katika Ukingo wa Magharibi na hilo linaashiria kushika kasi mapambano.