Hamas: Mauaji ya raia wa Kipalestina yanaonesha sura mbaya ya Israel

Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amesema kuwa, mauaji yanayofanywa kwa makusudi na askari wa Israel dhidi ya raia wa Kipalestina yanaonyesha sura mbaya ya wavamizi hao wanaoikalia Palestina kwa mabavu.

Katika mahojiano yake na kituo cha redio cha Saut al-Aqsa, Fouzi Barhoum ameongeza kuwa, matamshi yaliyotolewa na Waziri Mkuu wa Israel, Yair Lapid kuhusu mkono uliowazi wa jeshi wa kuwapiga risasi raia wa Palestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, ni ishara ya msisitizo wa wavamizi hao wa kutekeleza jinai za kupangwa.

Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel alitangaza Jumatano iliyopita kwamba hataruhusu kufunguliwa kesi dhidi ya mwanajeshi yeyote wa Israel aliyehusika na mauaji ya Wapalestina.

Msemaji wa Hamas ameongeza kuwa, kitendo hiki ni kukiri rasmi jinai ya kuwaua Wapalestina kwa damu baridi kabisa, mauaji ambayo yanafanywa na askari wa Israel katika ardhi yote ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Fouzi Barhoum amesema, jinai hizo hazilizuii taifa la Palestina kuendeleza mapambano na muqawama hadi ardhi yote ya Palestina itakapokombolewa na kurejea kwa wakimbizi wote katika nchi yao.

Msemaji huyo wa harakati ya Hamas amewaonya makamanda wa jeshi la utawala wa Kizayuni dhidi ya kuendeleza vitendo hivyo hatari na kusema kuwa, jamii ya kimataifa inapaswa kutekeleza wajibu wake wa kusimamisha jinai zinazofanyika dhidi ya ardhi, taifa na matukufu ya Wapalestina.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *