HAMAS: Msikiti wa Aqsa uko chini ya dhulma kubwa ya Wazayuni

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imesema kuwa, Msikiti wa al Aqsa (ambao ni Kibla cha Kwanza cha Waislamu) ni miongoni mwa nembo kuu ya Uislamu na kwamba mji mtakatifu wa Quds uliko Msikiti huo mtakatifu, daima umekuwa ukilengwa na maadui Wazayuni.

Ayad Fannunah, mmoja wa viongozi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema hayo katika tamasha lililobeba kaulimbiu ya “Msikiti wa al Aqsa uko Hatarini” kwamba, taifa la Palestina litaendelea na mapambano yake hadi utakapoangamizwa utawala wa Kizayuni na kukombolewa kila shibri ya ardhi ya Palestina.

Amesema, Msikiti wa al Aqsa unakabiliwa na hatari kubwa hivi sasa na uko chini ya dhulma ya kuchupa mipaka ya Wazayuni.

Kiongozi huyo mwandamizi wa HAMAS ametoa pongezi pia kwa wanamapambano wa kambi ya muqawama kutokana na operesheni zao katika kitovu cha mji wa Quds na kusisitiza kuwa, harakati ya HAMAS na brigedi za Izzuddin Qassam (tawi la kijeshi la harakati hiyo) itaendelea kuwasaidia wanamapambano wa Palestina wa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na mji wa Baytul Muqaddas.

Kiongozi huyo wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ametuma ujumbe pia kwa Itamar Ben-Gvir, mmoja wa wabunge wa Israel na kumwambia kamwe huwezi kulinda usalama wako wala wa walowezi wenzako wa Kizayuni.

Vile vile ametoa onyo kali akisema, kuanzia sasa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na mji wa Quds havitobaki salama tena.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *