Mjumbe mwandamizi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema kuwa, muqawama na mapambano ndio njia bora kabisa ya kuzikomboa ardhi za Palestina na kuifanya Palestina kuwa huru.
Ismail Ridhwan amesisitiza kuwa, jibu la Wapalestina kwa jinai za utawala ghasibu wa Israel unaokalia Quds kwa mabavu litakuwa ni mtutu wa bunduki.
Kiongozi huyo wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesisitiza kuwa, kudumishwa mapambano ndio njia na chaguo bora kabisa la kuzikomboa ardhi zote za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni maghasibu.
Aidha sambamba na kutoa wito wa kudumishwa muqawama na mapambano dhidi ya utawala bandia wa Israel, Ismail Ridhwan amesisitiza kuwa, hakuna njia ya mkato ya kuzikomboa ardhi za Palestina ghairi ya mapambano.
Harakati za Hamas na Jihadul Islami za Palestina zimekuwa zikilaani mara kwa mara mwenendo wa baadhi ya watawala wa Kiarabu wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel na kusisitiza kwamba, muqawama ndio njia pekee ya kuzikomboa ardhi za Palestina.
Utawala haramu wa Kizayuni wa Israel ambao unaungwa mkono kikamilifu na Marekani na washirika wake umeshadidisha njama na hujuma dhidi ya Palestina na maeneo yake matakatifu ambapo umedhamiria kubadilisha muundo wa kijiografia na kidemografia wa maeneo ya Palestina; ili kuyazayunisha maeneo hayo na kuhakikisha kwamba unazihodhi na kuzidhibiti kikamilifu ardhi za wananchi madhulumu wa Palestina.