Kiongozi mmoja mwandamizi wa Harakati ya Mapambano ya Kiisalamu ya Palestina HAMAS amesema kuwa, muqawama uko chini ya mwavuli wa uungaji mkono wa kivitendo wa Wapalestina na jambo hilo ndilo linalozidi kutia nguvu harakati za muqawama katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Kituo cha upashaji habari cha Palestina kimeripoti habari hiyo na kunukuu matamshi ya Mahmoud Mardawi, mmoja wa viongozi muhimu wa HAMAS akisema katika mahojiano na al Hurriya News kwamba, wanamapambano wa kambi ya muqawama katika maeneo ya Jenin, Tulkarm na Nablos hivi sasa wako chini ya mwavuli wa uungaji mkono na msaada mkubwa wa wananchi wa Palestina hasa wa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na wanatoa vipigo vikali na vya kuumiza kwa walowezi wa Kizayuni na wanajeshi madhalimu wa Israel.
Amesema, muqawama wa Palestina unapambana na siasa za kibeberu za ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika maeneo tofauti ya Ukingo wa M|agharibi wa Mto Jordan na jambo hilo linawatia kiwewe na hofu kubwa wanajeshi wa utawala wa Kizayuni kiasi kwamba kila kukicha wanaimarisha ulinzi katika maeneo ya kusini na kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Kiongozi huyo mkubwa wa Harakati ya Mapambano ya Kiisamu ya Palestina HAMAS pia amesema, uungaji mkono wa wananchi kwa kambi ya muqawama unafikisha ujumbe kwamba, taifa la Palestina limechagua muqawama na mapambano ya silaha kuwa ndiyo njia pekee ya kuweza kukomboa ardhi zao na kuwaokoa na ukatili wa utawala wa Kizayuni wa Israel.