HAMAS na Jihadul-Islami: Jinai za Israel hazina taathira yoyote kwa azma ya taifa la Palestina

Harakati za Hamas na Jihadul Islami za Palestina zimesisitiza kuwa, Jinai za Israel hazina taathira yoyote kwa irada na azma ya taifa la Palestina na kwamba, Wapalestina wanafungamana kikamilifu na chaguo la muqawama na mapambano dhidi ya utawala ghasibu wa Israel.

Taarifa ya Harakati za Hamas na Jihadul Islami za Palestina imetolewa kufuatia tukio la kuuawa shahidi kijana mdogo wa Kipalestina katika kitongoji kimoja magharibi mwa mji wa Jenin na kusisitiza kwamba, Wapalestina wanafungamana kikamilifu na chaguo la muqawama na mapambano dhidi ya utawala ghasibu wa Israel.

Hamas na Jihadul-Islami zimelaani vikali uvamizi wa mara kwa mara wa Wazayuni dhidi ya wananchi wa Palestina katika mji mtakatifu wa Quds, Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, Ukanda wa Gaza na dhidi ya ardhi za Palestina zilizoghusubiwa na kukaliwa kwa mabavu mwaka 1948.

Harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina imesisitiza kwa mara nyingine tena kwamba, jinai za utawala ghasibu wa Israel zinazidisha ari na irada ya muqawama na mapambano ya Wapalestina dhidi ya utawala huo ghasibu.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, hivi karibuni Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ilisisitiza kuwa, Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na mji wa Jenin vimekuwa hifadhi na nguzo ya muqawama.

Vijana na makundi ya muqawama ya Palestina yametangaza mara kadhaa kuwa, mapambano baina yao na utawala haramu wa Israel unaoikalia Quds kwa mabavu yako wazi kote Palestina na ni mapambano ya pande zote.

Inaelezwa kuwa, muqawama katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan umepiga hatua kwa kumiliki silaha sambamba na kutekelezwa operesheni za kutumia silaha baridi na kuwadhibiti Wazayuni.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *