Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imetangaza kuwa inataka kuwa na uhusiano imara na Syria ikiwa ni katika fremu ya uamuzi wa harakati hiyo wa kuanzisha tena uhusiano na Damascus.
Katika taarifa iliyoitoa leo Alhamisi, Hamas imelaani mashambulizi ya anga ya utawala wa Kizayuni huko Syria na kusisitiza kuwa harakati hiyo iko imara katika kukabiliana na utawala wa Kizayuni dhidi ya Syria. Taarifa ya Hamas imeongeza kuwa, “Tunafuatilia kwa makini kuendelea chokohoko na hujuma za utawala wa Kizayuni kwa kulipua mabomu, kuua raia na kuharibu miundombinu ya nchi ndugu yetu Syria na kushadisishwa jitihada za utawala huo za kuidhoofisha, kuigawa na kuisambaratisha Syria.”
Harakati ya Muqawama ya Hamas imeashiria namna inavyofuatilia njama za kuiweka mbali Syria na nafasi yake athirifu ya kihistoria khususan katika kufungamana na malengo ya Palestina na kusisitiza kuwa: Syria ililikumbatia taifa la Palestina na makundi ya muqawama ya nchi hii kwa miongo kadhaa; ndio maana inaona ni jukumu na wajibu kwake kuwa bega kwa bega na Syria katika hali ya hujuma na kushambuliwa kidhulma nchi hiyo”.
Utawala wa Kizayuni miaka ya karibuni umetekeleza hujuma na mashambulizi mbalimbali ya anga dhidi ya Damascus na maeneo mbalimbali ya Syria; mashambulizi ambayo mara nyingi yamezuiwa kwa wakati na ngao ya ulinzi wa anga ya Syria.