HAMAS: Utawala wa Kizayuni umeshindwa kukabiliana na muqawama Ukingo wa Magharibi

Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema kuwa, jinai za utawala wa Kizayuni za kuwaua kigaidi wanamapambano wa Palestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan hazitapunguza kasi ya kuimarika muqawama wa wananchi wa Palestina.

Jana Jumapili, utawala wa Kizayuni ulimuua kigaidi Tamer al-Kilani, mmoja wa makamanda wa muqawama wanaojulikana kwa jina la Pango la Simba (‘Arin al Usud) kwa kutumia pikipiki iliyokuwa imetegwa mabomu na kuegeshwa kando ya barabara.

Tovuti ya habari ya al ‘Ahd imemnukuu Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS, Abdul Latif al-Qanoo akisema kuwa, utawala wa Kizayuni umeshindwa kukabiliana na muqawama wa wananchi wa Palestina huko Jenin, Nablos na miji mingine ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na ndio maana umeamua kutumia vibaraka wake wa siri kuua wanamapambano wa Palestina.

Amesema, jinai ya Israel ya kumuua kigaidi Tamer al-Kilani ni ushahidi wa kushindwa utawala wa Kizayuni kukabiliana na wanamapambano wa Palestina na mashujaa wa ‘Arin al Usud (Pango la Simba) huko Nablos. Ameongeza kuwa, jinai za Wazayuni za kuwaua kigaidi Wapalestina haziwezi kuzima muqawama wa wananchi mashujaa wa Palestina katika Ukiingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Msemaji huyo wa HAMAS ameonya pia kuwa, ‘Arin al Usud na muqawama utaendelea katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na hautokaa kimya baada ya Wazayuni kumuua kigaidi, kamanda Tamer al-Kilani.

Amesema, mbinu zote ambazo hadi hivi sasa zimetumiwa na utawala wa Kizayuni za kujaribu kukwamisha operesheni za muqawama, zimefelishwa na msimamo imara wa wananchi wa Palestina.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *