Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imesisitiza kuwa, vita dhidi ya utawala haramu wa Israel vitaendelea mpaka pale mateka wote wa Kipalestina wanaoshikiliwa na utawala huo ghasibu watakapoachiliwa huru.
Hayo yameelezwa na Zaher Jabarin, afisa wa Hamas anayeshughulikia faili la mashahidi na mateka wa Palestina na kueleza kwamba, harakati hiyo haitapata utulivu na amani madhali kuna Wapalestina wanaoshikiliwa mateka katika magereza ya utawala vamizi wa Israel.
Afisa huyo wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ametoa mwito wa kuungwa mkono kwa hali na mali mateka wa Kipalestina ambao amewataja kama mashujaa wa Palestina na dunia kwa ujumla kutokana na misimamo yao thabiti waliyoionyesha.
Kamati ya Dharura yenye mfungamano na harakati ya mateka wa Kipalestina katika magereza ya utawala ghasibu wa Israel imekuwa ikisisitiza kuwa, Intafadha ya wafungwa wa Kipalestina katika magereza ya Israel haitosita mpaka pale matakwa ya mateka na wafungwa wa Kipalestina yatakapotekelezwa kikamilifu.
mateka
Katika miezi ya hivi karibuni, utawala haramu wa Israel kupitia maafisa wake wa magereza, umeshadidisha ukandamizaji wake dhidi ya wafungwa wa Kipalestina, unyama ambao umekabiliwa na malalamiko makubwa ya walimwengu kieneo na kimataifa.
Ukandamizaji huo wa utawala ghasibu wa Israel dhidi ya mateka Wapalestina umepelekea wananchi wa Palestina wafanye maandamano mara kadhaa ya kutangaza uungaji mkono wao kwa wafungwa hao, huku baadhi ya wafungwa wenyewe wakifanya mgomo wa kula kulaani mbinyo dhidi yao.