Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imewatahadharisha Wazayuni kuhusu kuendelea kuuhujumu Msikiti wa al Aqsa na kuwatolea mwito Wapalestina kuhudhuria kwa nguvu zote na kwa mshikamano katika msikiti huo.
Msikiti wa al Aqsa ambao ni nembo kuu ya utambulisho wa Kiislamu na wa Palestina katika mji wa Baitul Muqaddas umekuwa ukilengwa na kukabiliwa na mashambulizi na hujuma za uharibifu za utawala ghasibu wa Israel.
Muhammad Hamadeh msemaji wa harakati ya Hamas katika mji wa Quds amewataka Wapalestina kudhihirisha mshikamano wao na kuhudhuria kwa wingi katika maeneo na uwanja wa Msikiti wa al Aqsa.
Hamadeg amesema: “Tunapitia kipindi nyeti hivi sasa; hali ambayo inatoa ulazima wa kukusanyika Wapalestina wote, kuwepo siku zote na kwa wingi katika eneo la msikiti mtakatifu wa al Aqsa ambao ni kibla cha kwanza cha Waiislamu. Hili ni jukumu letu sote.” Ameongeza kuwa, kuwepo kwa wingi Wapalestina katika Msikiti wa al Aqsa kutazuia hujuma na mashambulizi ya maghasibu wa Kizayuni huko Baitul Muqaddas na katika msikiti huo mtakatifu.
Wakati huo huo msemaji wa Hamas amesisitiza kuwa, maghasibu Wazayuni karibuni hivi wataungua katika moto utakaosababishwa na hujuma na mashambulizi yao dhidi ya Msikiti wa al Aqsa na kuongeza kuwa: Ben-Gvir Myahudi mwenye misimamo ya kufurutu ada wa Israel atakabiliwa na hatima mbaya sana kuliko ile iliyowakumba Wayahudi wenzake wenye misimamo mikali kama yake.