Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imeukosoa Umoja wa Mataifa kwa kupitisha maazimio kadhaa dhidi ya utawala wa Kizayuni bila ya kufikiria njia za kivitendo za kuwezesha utekelezaji wake.
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepiga kura ya kuunga mkono mpango uliowasilishwa na Palestina, kuhusiana na kutolewa uamuzi wa kisheria na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC iliyoko The Hague kuhusu asili na hali ya kisheria uliyonayo utawala ghasibu wa Kizayuni wa Israel katika ardhi ya Palestina.
Kwa mujibu wa chaneli ya habari ya Al Jazeera, Hamas imeeleza katika taarifa iliyotoa kuhusiana na azimio jipya lililopitishwa dhidi ya utawala haramu wa Israel katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ya kwamba, azimio hilo, nalo pia linaongezwa kwenye mfululizo wa maazimio kadhaa ya kimataifa ambayo hayana njia za kivitendo za utekelezaji kwa ajili ya kuwashinikiza wakaliaji ardhi kwa mabavu.
Katika taarifa yake hiyo Hamas imesisitiza kuwa, maadamu Marekani, ambayo ni mshirika wa utawala unaoikalia Quds kwa mabavu, ingaliko katika uchukuaji hatua na inaendelea kuvipa kinga vitendo vya Wazayuni, maazimio hayo yatabaki kuwa wino tu ulioandikwa kwenye karatasi na hayatakuwa na athari yoyote ya kivitendo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Hamas, maamuzi rasmi ya kidiplomasia ambayo chimbuko lake ni udhaifu wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, yanatokana na kushindwa maamuzi hayo yanayopitishwa, kukabiliana ipasavyo na wazayuni maghasibu na yanadhihirisha udhaifu mkubwa wa miundo yake ya kiutendaji.
Ripoti zinaeleza kuwa, Mamlaka ya Ndani ya Palestina imetoa taarifa kuhusiana na azimio la Umoja wa Mataifa dhidi ya utawala wa Kizayuni ikisisitiza kuwa, kura ya ‘ndiyo’ ya Umoja wa Mataifa kwa azimio hilo ni ishara ya uungaji mkono wa walimwengu kwa watu wa Palestina na haki zao za kihistoria.