HAMAS yalaani kitendo cha askari wa Israel cha kuwakashifu Wapalestina kwa kuwavua nguo hadharani

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imelaani kitendo cha wanajeshi wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel cha kuwalazimisha kuvua nguo Wapalestina wapatao 100 waliowakamata; na kuwakashifu kwa kuwaweka hadharani katika barabara za Ukanda wa Gaza wakiwa wamebaki na nguo za ndani tu.

Askari wa jeshi la utawala wa Kizayuni walirekodi mikanda ya vidio inayowaonyesha wanaume Wapalestina waliowakamata na kuisambaza kwa wingi kwenye mitandao ya kijamii.
Vidio hizo ambazo zilithibitishwa uhakika wake baada ya kuibuka siku ya Alkhamisi, zinaonyesha watu hao wakiwa wamekaa barabarani mahali fulani kaskazini mwa Gaza huku wakitazamwa na wanajeshi kadhaa wa Kizayuni.
Izzat  al-Rishq, mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya Hamas ametoa taarifa ya kulaani kitendo hicho cha kishenzi na cha udhalilishaji kilichofanywa na jeshi la Kizayuni na kuyahimiza mashirika ya kimataifa ya haki za binadamu kuchunguza suala hilo.

Sehemu moja ya taarifa hiyo imesema: “kuwavua nguo zao kwa namna ya kuwadhalilisha ni jinai ya wazi ya Wazayuni ya kulipiza kisasi kwa raia wetu wasio na ulinzi kutokana na vipigo wanavyopata askari na maafisa wake kwa wapiganaji wa Muqawama wa Palestina”.

Taarifa hiyo imeendelea kueleza, “tunaubebesha utawala vamizi (wa Kizayuni) dhima ya maisha na usalama wao, na tunatoa wito kwa taasisi na mashirika yote ya haki za binadamu na taasisi za masuala ya kibinadamu kuingilia kati.”
Licha ya kutobainishwa wazi sababu ya kutiwa nguvuni Wapalestina hao na mahali walikopelekwa, msemaji wa jeshi la utawala haramu wa Israel alidai kuwa wanawashikilia raia hao wa Palestina ili kuwahoji na kuona nani ana uhusiano na Hamas na nani hana uhusiano na harakati hiyo ya Muqawama. Msemaji huyo wa jeshi la Kizayuni hakuzungumza moja kwa moja kuhusu vidio hiyo, lakini alisema mamia ya washukiwa wamehojiwa hadi sasa na kwamba eti wengi walijisalimisha katika muda wa saa 48 zilizopita.

Wataalamu wa sheria wanasema, kuwatendea namna hiyo watu waliokamatwa ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa.

Mamia ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza unaozingirwa na Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu wametiwa nguvuni na kuwekwa kizuizini tangu Hamas ilipoanzisha operesheni ya kushtukiza ya Kimbunga cha Al-Aqsa mnamo Oktoba 7 ili kukabiliana na ukatili wa miongo kadhaa wa utawala dhalimu wa Kizayuni wa Israel.

Tangu wakati huo hadi sasa, jeshi la Kizayuni limeshawaua shahidi zaidi ya watu 17,400 huko Gaza wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *