Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS kwa mara nyingine tena imesisitiza kwamba, inapinga kuanzishwa uhusiano wa aina yoyote na utawala haramu wa Israel.
Taarifa iliyotolewa na Kituo cha Upashaji Habari cha Palestina imeeleza kuwa, HAMAS inakanusha madai ya baadhi ya vyombo vya habari kwamba, imeafiki suala la kuanzishwa uhusiano wa kawaida baina ya Uturuki na utawala ghasibu wa Israel.
Sehemu nyingine ya taarifa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imesisitiza kuwa, harakati hii kwa mara nyingine tena inatangaza wazi na bayana upinzani wake dhidi ya mbinu zote za kuanzishwa uhusiano wa kawaida na utawala vamizi wa Israel.
Aidha HAMAS imeeleza kuwa, harakati hiyo katu haiafiki na wala haiko tayari kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo, kwani siasa za Wazayuni zinapingana na misingi ya kitaifa na maslahi ya wananchi wa Palestina, mataifa ya Kiarabu na ya Kiislamu.
Septemba mwaka juzi (2020), Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Imarati na Bahrain walisaini mkataba wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel katika hafla iliyofanyika katika Ikulu ya White House mjini Washington kwa usimamizi wa aliyeko Rais wa Marekkani Donald Trump.
Baada ya hapo Sudan na Morocco nazo zikafuata mkumbo huo na kutangaza kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo haramu, uamuzi ambao umeendelea kulalamikiwa na kulaaniwa na wapenda haki kote ulimwenguni huku kukishuhudiwa maandamano hasa katika mataifa ya Morocco na Sudan ya kupinga usaliti huo.