Sambamba na kutimia mwaka wa 29 tangu yaliposainiwa Makubaliano ya Oslo, Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (Hamas) imeitaka Mamlaka ya Ndani ya Palestina itangaze kufutwa makubaliano hayo ya nakama.
Makubaliano ya Oslo yalitiwa saini tarehe 13 Septemba 1993 kati ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel na Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO); ambapo iliafikiwa kwamba masuala kama hali ya Baitul Muqaddas, wakimbizi Wapalestina, vitongoji vya walowezi wa Kizayuni, masuala ya kiusalama pamoja na kile kinachotajwa kama uainishaji mipaka yangetatuliwa kupitia makubaliano hayo, lakini mazungumzo ya zaidi ya miaka 20 yaliyofanyika baina ya pande hizo mbili hayajawa na matunda yoyote kwa wananchi wa Palestina.
Kwa mujibu wa tovuti ya Shahab News, harakati ya Hamas imetoa taarifa ikiashiria kuendelezwa muqawama uliosambaa pande zote za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan dhidi ya utawala wa Kizayuni pamoja na mapambano ya wafungwa wa Kipalestina katika jela za utawala huo ghasibu na kusisitiza kuwa, matukio hayo yanadhihirisha ukweli kwamba muqawama na aina zake zote ndilo chaguo kuu la taifa la Palestina kwa ajili ya kuikomboa ardhi hiyo, kupatikana haki ya kurejea wakimbizi na haki ya Wapalestina kujiamulia mustakabali wao.
Aidha, sambamba na kutimia mwaka wa 29 wa kusainiwa mkataba wa nakama wa Oslo, Harakati ya Hamas imeitaka Mamlaka ya Ndani ya Palestina iyafute makubaliano hayo iliyosaini na utawala wa Kizayuni na kusimamisha ushirikiano wa kiusalama na kiuchumi na Wazayuni.
Hamas imesisitiza pia ulazima wa mamalaka ya ndani ya Palestina kuchukua hatua za haraka za kutangaza kutoutambua utawala wa Kizayuni wa Israel.