Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imelaani vikali hatua ya serikali ya Australia ya kuitambua harakati hiyo ya muqawama inayopigania ukombozi wa Palestina kuwa ni kundi na kigaidi.
Taarifa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ikmesisitiza kuwa, Israel ndio inayopaswa kutangazwa kuwa utawala wa kigaidi kutokana na jinai zake za kila leo dhidi ya wananchi wa Palestina.
Hazim Qassim, msemaji wa HAMAS amesema kuwa, uamuzi huo wa serikali ya Australia unakinzana wazi kabisa na sheria na maazimio yote ya kimataifa ambayo yameitambua haki ya taifa la Palestina katika kupambana na kukabiliana na utawala vamizi wa Israel.
Kiongozi huyo ameongeza kuwa, HAMAS ni harakati ya kitaifa ya ukombozi ambayo inaendesha mapambano dhidi ya wavamizi na kwa mujibu wa sheria za kimataifa, sasa vipi harakati kama hii itambuliwe kuwa ni kundi la kigaidi, ilihali utawala wa Israel ambao unafanya mauaji kila siku hata dhidi ya watoto wachanga hauonekani kama unafanya vitendo vya kigaidi?
Karen Andrews, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Australia ametangaza kuwa, serikali ya nchi hiyo itaiweka harakati ya Hamas katika orodha ya makundi ya kigaidi.
Hatua ya Australia ambayo imefanyika kwa ajili ya kuuunga mkono utawala haramu wa Israel imechukuliwa katika hali ambayo, katika majuma ya hivi karibuni mashirika ya kutetea haki za binadamu likiwemo la Amnesty International yakiwa na lengo la kuiunga mkono Palestina yametangaza kuwa, Israel ni utawala wa ubaguzi wa rangi (apartheid).