Harakati mbili za mapambano ya Kiislamu (muqawama) Palestina za Hamas na Jihad Islami zenye makao yake katika Ukanda wa Gaza zimelaani vikali ziara inayoendelea nchini Bahrain ya rais wa utawala ghasibu wa Israel.
Afisa mwandamizi wa Hamas Basim Naim na msemaji wa Jihad Islami Tariq Salmi walilaani safari hiyo siku ya Jumapili saa chache baada ya Isaac Herzog kuwa rais wa kwanza wa utawala bandia wa Israel kuwahi kusafiri hadi katika ufalme huo mdogo wa Kiarabu ulio katika Ghuba ya Uajemi.
Bahrain ilitia saini makubaliano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel chini ya usimamizi wa Marekani katika Ikulu ya White House mnamo Septemba 2020. Tangu wakati huo, tawala za Manama na Tel Aviv zimekuwa zikijaribu kuimarisha uhusiano huku Wapalestina na wafuasi wao wa kieneo na kimataifa wakiutaja uhusiano huo kuwa ni usaliti kwa harakati ya kupigania ukombozi wa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Israel.
Naim ameitaja ziara hiyo kuwa ya “udhalilishaji,” na akashutumu hatua ya Mfalme wa Bahrain Hamad bin Isa Al Khalifah ya kumkaribisha mkuu wa utawala wa kibaguzi, ambaye anaongoza muundo mkubwa zaidi wa kigaidi ulimwenguni.
Amekumbusha kuwa mfalme wa Bahrain alikuwa anampokea rais wa Israel huku wanajeshi wa utawala ghasibu wa Israel wakiendelea kuwaua kiholela Wapalestina katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na kusema kutokana na ukatili mbaya wa utawala huo ghasibu, damu ya vijana hao wa Kipalestina imeanza kutiririka kama “mto”.
Naim aliongeza kuwa ziara hiyo pia iliambatana na ukiukwaji unaoendelea wa Israel dhidi ya maeneo matakatifu ya ulimwengu wa Kiislamu, hasa Msikiti wa al-Aqsa – eneo la tatu kwa utakatifu katika Uislamu.
Afisa huyo wa Hamas alisema kwa kujipendekeza kwa Tel Aviv, watawala wa Bahrain wanajaribu kulazimisha matakwa yao wa Wabahrain waliowengi wanaopinga uhusiano na Israel. Hii ni katika hali ambayo “watawala hupata uhalali wao kutoka kwa wananchi na ” sio kupitia kujikurubisha kwa maadui wa mataifa”.
Wakati huo huo masemaji wa Jihad Islami, ameitaja safari ya Herzog nchini Bahrain kuwa ni hatua inayolenga kupuuza ukatili na vitendo vya kigaidi vya utawala ghasibu wa Israel.
Salmi amewapongeza wananchi wa Bahrain kwa kulalamikia safari hiyo, akitoa wito kwa mataifa yote ya Kiislamu na Kiarabu kupaza sauti zao dhidi ya kila hali ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Israel.