Makumi ya Waislamu wakimbizi wa jamii ya Rohingya kutoka Myanmar waliodhoofu kwa njaa na kiu wamepatikana ufukweni mwa pwani ya jimbo la Aceh kaskazini ya Indonesia baada ya wiki kadhaa za kutaabika na kutangatanga baharini.
Kwa mujibu wa mkuu wa Polisi ya eneo hilo Rolly Yuiza Away, kundi la Waislamu hao wanaume 58 liliwasili mapema jana Jumapili kwenye ufukwe wa pwani ya Indrapatra iliyoko Ladong, kijiji cha wavuvi katika wilaya ya Aceh Besar.
Wanakijiji waliowaona Waislamu hao waliokuwa kwenye boti ya mbao iliyochakaa waliwasaidia kufika nchi kavu na kisha kuripoti kuwasili kwao kwa mamlaka husika.
Kamanda wa Polisi Away amesema, watu hao walikuwa wamedhoofu sana kutokana na njaa na upungufu wa maji mwilini na baadhi yao ni wagonjwa baada ya safari ndefu na ngumu baharini.
Siku ya Ijumaa, Umoja wa Mataifa na asasi zingine za kimataifa zilizitolea wito nchi za Asia Kusini wa kuwaokoa takriban watu 190, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto, wanaoaminika kuwa wakimbizi wa jamii ya Rohingya, waliokuwa kwenye mashua ndogo ambayo imekuwa ikielea kwa wiki kadhaa katika Bahari ya Andaman.
Haijajulikana kama wakimbizi hao 58 waliowasili Indonesia ni sehemu ya watu hao 190 walioripotiwa au la.
Itakumbukwa kuwa, Agosti 2017, zaidi ya Waislamu laki saba wa jamii ya Rohingya walilazimika kuhama makazi yao nchini Myanmar na kukimbilia kwenye kambi za wakimbizi nchini Bangladesh ili kutafuta hifadhi na kunusuru maisha yao, baada ya jeshi la Myanmar, likishirikiana na Mabudha wenye chuki za kidini, kuanzisha operesheni ya kuwaondoa kwa nguvu Waislamu hao kwa kisingizio cha mashambulizi yaliyofanywa na kundi moja la waasi. Vikosi vya jeshi la Myanmar vimehusika na jinai mbalimbali dhidi ya Waislamu Warohingya zikiwemo za ubakaji wa halaiki, mauaji na kuchoma moto maelfu ya nyumba.