Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon Sheikh Naim Qassem ameonya kuwa harakati hiyo ya muqawama (mapambano ya Kiislamu) itauadhibu utawala haramu wa Israel na kuurudisha kwenye fahamu zake endapo utafanya upumbavu wowote katika suala la makubaliano ya kuweka mipaka ya baharini na Lebanon.
Kiongozi huyo nambari mbili katika Hizbullah alitoa kauli hiyo Alkhamisi na kuongeza kwamba Hizbullah iko tayari kukabiliana na utawala ghasibu wa Israel. Aidha amesema ni nguvu na umoja wa Lebanon ndio umeiruhusu nchi hiyo iliyokumbwa na mzozo kushughulikia matatizo yake na pia kuidhaminia kuainishwa mipaka ya baharini.
Hivi karibuni, Lebanon na utawala wa Kizayuni wa Israel zilitiliana saini makubaliano ya mpaka wa baharini kwa upatanishi wa Marekani. Hivi sasa lakini Benjamin Netanyahu anadai kuwa hatoheshimu makubaliao hayo.
Kwingineko katika matamshi yake, Sheikh Qassem, naibu wa Seyyed Hassan Nasrallah, Katibu Mkuu wa Hizbullah amesema Marekani inawakandamiza watu wote duniani.
Shirika la Habari la Sputnik limemnukuu Sheikh Qassem akisema, “Hatutakubali kamwe kuwa chini ya amri ya Marekani au kutii amri zake. Mustakabali utathibitisha kwamba Marekani haitaweza kutekeleza mipango yake katika eneo ambalo kuna muqawama au mapambano na pia kuna mataifa ambayo hayakubali utawala wa kibeberu wa Marekani.”
Amesema kuwa Marekani inakabiliana na Hizbullah kutokana na msimamo imara wa Hizbullah wa kupambana na utawala haramu wa Israel na kuongeza kuwa, “Israel iliundwa na nchi za Magharibi kuwa chombo chake na kupitia kwayo kutawala mustakabali na hatima ya eneo hili.”
Akizungumzia uchaguzi wa karibuni katika utawala wa Israel, Sheikh Qassem amesisitiza kuwa “uchaguzi huu hautabadilisha chochote. Kuna tatizo moja nalo ni; kuna mvamizi katika eneo letu anaitwa utawala wa Israel. Kwa hiyo, haijalishi ni nani waziri mkuu.”
Naibu wa Sayyed Hassan Nasrallah amevitaja vitisho vya Benjamin Netanyahu kuwa si chochote zaidi ya “bomu la sauti” ambalo halina athari.