Dodoma. Hospitali ya Benjamin Mkapa imezindua mtambo wa kuzalisha hewa tiba ya Oxygen utakaozalisha mitungi ya gesi 400 kwa siku.
Mtambo huo umezinduliwa leo Ijumaa Julai Mosi, 2022 na jijini Dodoma na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu huku akimwagia sifa hospitali hiyo kwa utoaji huduma bora na kuahidi kuipandisha hadhi kuwa ya Taifa.
“Popote nitakapokwenda nitasema Hospitali ya Benjamin Mkapa haininyimi usingizi tofauti na hospitali nyingine, kila wakati napokea ujumbe wa simu na barua juu ya huduma bora na tiba na watumishi kutoka kwa wagonjwa”amesema
Waziri Ummy ameuagiza uongozi wa hospitali hiyo kukamilisha ujenzi wa majengo muhimu ya tiba ikiwamo wodi ya magonjwa ya moyo na saratani ili kukamilisha azma hiyo hata kabla ya mwaka 2025.
Awali Mkurugenzi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa Dk Alphonce Chandika akizungumzia mtambo huo uliogharimu Sh1.1 bilioni, amesema utasaidia upatikanaji wa gesi kwenye hospitali hiyo na hospitali za mikoa ya karibu ikiwamo Manyara, Singida, Mvumi, Singida na ya Mkoa wa Dodoma.
Amesema Hospitali hiyo awali ilitumia Sh10 milioni kununua mitungi ya gesi 200 kwa mwezi ambapo baada ya kuibuka kwa Ugonjwa wa Uviko-19 hospitali hiyo ililazimika kutumia kiasi hiko cha fedha kununua mitungi 200 kwa siku.
Amesema mfumo wa mtambo huo uliohusisha manunuzi ya gari la kusambazia mitungi ya gesi, mtambo wenyewe na jengo umegharimu Sh1.5 bilioni.