HRW: Maadamu Israel haiadhibiwi, mashambulio dhidi ya Gaza yataendelea

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema, kutoadhibiwa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel ndiko kunakoufanya utawala huo uendeleze hatua unazochukua.

Katika taarifa kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter, Human Rights Watch imesema, Wapalestina zaidi ya 40, wakiwemo watoto 15 wameuawa katika vita vya siku tatu za karibuni kati ya utawala wa Kizayuni na muqawama wa Palestina Gaza; na maadamu hakuna habari yoyote ya utoaji adhabu, uzushaji hali ya wasiwasi wa aina hii utaendelea pia.

Shirika hilo la kimataifa la kutetea haki za binadamu limeongezea kwa kusema: mzunguko huu wa kuzusha hali ya wasiwasi na mvutano utaendelea maadamu hakuna utoaji adhabu, maadamu Gaza inabaki kuwa jela ya eneo la wazi na madamu ubaguzi wa rangi wa apathaidi wa Israel hautoweki.

Duru mpya ya mashambulio ya kinyama ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza ilianza siku ya Ijumaa iliyopita kwa mauaji ya Tayseer Al-Jaabari, kamanda wa ngazi ya juu wa Sarayal-Quds, tawi la kijeshi la Harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina.

Wakati Wazayuni walikuwa wamedai kwamba mashambulio hayo yangeendelea kwa muda wa wiki nzima, baada ya kupita siku tatu, utawala haramu wa Israel uliafiki kusitisha mapigano kwa upatanishi wa Misri sambamba na kukubali kikamilifu masharti yaliyotolewa na harakati ya Jihadul-Islami.

Katika siku tatu hizo za mapigano, makundi ya muqawama ya Palestina yalijibu hujuma za kinyama za utawala wa Kizayuni kwa kuvurumisha mamia ya makombora yaliyolenga miji na vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu hususan Tel Aviv na uwanja wa ndege wa Ben Gurion.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *