Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema serikali ya Marekani imepuuza kutoa fidia kwa Wairaq walioteswa na askari wa jeshi la nchi hiyo.
Wakati wa vita vyake vya muda mrefu nchini Iraq, Marekani imeua raia wengi na kutesa idadi isiyohesabika ya washukiwa bila kuwafungulia mashtaka katika magereza yake kadhaa likiwemo la Abu Ghuraib.
Kwa mujibu wa Isna, Human Rights Watch imetangaza katika ripoti yake kwamba nyaraka za shirika hilo na mashirika mengine ya kimataifa zinaonyesha kuwa vitendo vingi vya ukiukaji wa haki za binadamu vilifanywa katika jela ya Abu Ghuraib nchini Iraq na jela nyingine zilizokuwa chini ya utawala wa Marekani katika nchi hiyo.
Ripoti hiyo imeeleza kuwa licha ya ushahidi uliorekodiwa wa mateso, ukatili na unyanyasaji dhidi ya Wairaq uliofanywa na wanajeshi wa Marekani, Marekani imepuuza suala la kutoa fidia au msaada kwa Wairaq waliofikwa na mateso hayo.
Kwa hiyo wahasiriwa wa mateso na ukatili huo hawajapokea fidia yoyote, licha ya kutoa ushahidi kwamba Wamarekani waliwatendea vibaya.
Ripoti ya Human Rights Watch imebainisha pia kuwa baada ya kuivamia Iraq mwaka 2003, Marekani na washirika wake waliwakamata na kuwaweka kizuizini Wairaq wapatao 100,000 kati ya mwaka 2003 hadi 2009.
Mnamo Machi 20, 2003, George W. Bush, rais wa wakati huo wa Marekani, alichukua hatua ya upande mmoja na ya kinyume cha sheria kwa ushirikiano na Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza Tony Blair kwa kuamuru kuanzishwa mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iraq bila idhini ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Baada ya hapo, majeshi ya Marekani na Uingereza yalianzisha vita vikubwa vilivyoiteketeza Iraq na kuua maelfu ya watu nchini humo…/