Jumanne usku ya tarehe 30 Julai 2024, Ismail Haniyeh Kiongozi wa Tawi la Kisiasa la Harakati ya HAMAS ameuawa shahidi akiwa na mlinzi wake mmoja hapa Tehran. Ufuatao hapa chini ni wasifu kwa muhtasari wa maisha yake.
Ismail Haniyeh alizaliwa mwaka 1962 katika kambi moja ya wakimbizi ya Ukanda wa Ghaza. Ukata na njaa iliyotokana na kukaliwa kwa mabavu ardhi za Palestina kulikofanywa na utawala wa Kizayuni kuliambatana naye tangu wakati wa utotoni kabisa wa maisha yake. Wakati Israel ilipoanza kuikalia kwa mabavu Ghaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, Haniyeh alionja pia uchungu wa kukaliwa kwa mabavu kikamilifu ardhi za Wapalestina.
Ismail Haniyeh alisoma katika skuli ya Umoja wa Mataifa, akaendelea na masomo yake katika Chuo Kikuu cha Ghaza, akawa mkuu wa Chama cha Wanachuo na muda wote alikuwa mstari wa mbele katika harakati za kupambana na utawala vamizi wa Kizayuni.
Ismaiil Haniyeh alikuwa mmoja wa vijana ambao walikuwa na mchango mkubwa katika Intifadha ya Kwanza ya Wapalestina na mwaka 1987 alionja pia machungu ya jela za utawala wa Kizayuni. Alijiunga na HAMAS wakati huo wa Intifadha ya Kwanza na kufungwa jela. Baada ya kukaa jela kwa muda wa miaka mitatu, Haniyeh na wanamapambano wengine wa HAMAS walibaidishwa na kupelekwa Lebanon. Huko Lebanon pia aliendelea na mapambano dhidi ya Wazayuni.
Ilikuwa ni mwaka 1993 wakati Haniyeh aliporejea Ghaza, na kwa muda fulani akawa Rais wa Chuo Kikuu cha Ghaza. Katika kipindi cha miaka yote hiyo alikuwa na uhusiano wa karibu na Sheikh Ahmad Yasin, mwasisi wa harakati ya HAMAS na baada ya shahid Ahmad Yasin kuachiliwa huru kutoka jela, Haniyeh alikuwa mkuu wa ofisi yake. Israel ilijaribu kuwaua kigaidi Ahmad Yasin na Haniyeh kwa pamoja, lakini jaribio hilo lilifeli na wanapambano hao wawili walijeruhiwa tu katika shambulio hilo.
Baada ya kuanza Intifadha ya Pili, Israel iliua sehemu kubwa ya viongozi na kizazi cha kwanza cha HAMAS na hivyo kutoa nafasi ya kizazi cha baadaye cha harakati hiyo kama vile Ismail Haniyeh kushika hatamu za uongozi.
Katika kipindi hicho, Israel ililazimika kukimbia kwenye Ukanda wa Ghaza, na hiyo ilikuwa ni fursa nzuri kwa Haniyeh kuiongezea nguvu zaidi na kwa haraka HAMAS na kwa kushirikiana na watu kama Muhammad Dhaif na Brigedi za Izuddin Qassam, waliweza kuimarisha sana nguvu za HAMAS katika safu za wananchi.
Baada ya kufanyika uchaguzi wa kwanza wa Bunge la Palestina, harakati ya HAMAS kwa uongozi wa Ismail Haniyeh, ilipata wingi wa viti na Haniyeh akawa Waziri Mkuu wa Palestina. Tab’an kwa uungaji mkono kamili wa Marekani, Israel haikuruhusu kabisa kuundwa serikali yenye nguvu ya Palestina na imeuwekea Ukanda wa Ghaza mzingiro wa pande zote tangu mwaka huo hadi hivi sasa.
Katika kipindi chote cha uongozi wa Haniyeh huko Ghaza, Israel imefanya mara chungu nzima majaribio ya kumuua mwanamapambano huyo lakini imefeli na nguvu za HAMAS zimekuwa zikiongezeka siku baada ya siku na katika vita vya 2014, harakati hiyo iliionesha Israel kuwa, haina uwezo tena wa kukabiliana na nguvu za kijeshi za HAMAS.
Umaarufu na mapenzi ya wananchi wa Palestina kwa Haniyeh yaliongezeka zaidi na zaidi na mwaka 2017 alichaguliwa kuwa Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya HAMAS. Mara chungu nzima Israel ilijaribu kumzuia Haniyeh kuingia katika Ukanda wa Ghaza, na hata mara moja ilifanya jaribio la kumuua akiwa katika kivuko cha Rafah lakini jaribio hilo la kigaidi lilifeli. Hivyo viongozi wakuu wa HAMAS waliamua kwamba, Ismail Haniyeh aondoke kabisa katika Ukanda wa Ghaza na aendeleze harakati zake nje ya Palestina. Lakini Israel iliona imalizie hamaki zake kwa ukatili wa kuua watu wa familia ya Ismail Haniyeh kwenye Ukanda wa Ghaza. Tab’an mauaji hayo yaliongeza tu mapenzi ya wananchi wa Palestina kwa Ismail Haniyeh na hata baada ya kuuawa kwake shahidi, athari za mchango mkubwa wa kiongozi huyo wa HAMAS zinaendelea kuonekana.