Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu (ICJ) imepokea rasmi ombi la Umoja wa Mataifa la kutaka maoni ya ushauri kutoka kwa chombo hicho juu ya taathira za Israel kughusubu na kukaliwa kwa mabavu ardhi za Palestina.
ICJ inatazamiwa kuandaa orodha ya mataifa na mashirika ambayo yatawasilisha taarifa za maandishi kwenye mahakama hiyo iliyoko mjini Hague nchini Uholanzi, kuhusu ombi hilo la UN.
Hata hivyo taatifa ya ICJ haijatoa maelezo ya kina kuhusu muda wa kuanza na kufanyika kwa vikao hivyo. Hata hivyo mchakato wa mafaili ya namna hii huchukua miezi kadhaa.
Disemba 31 mwaka uliomalizika, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, kwa kupitisha azimio, lilitaka maoni ya ushauri ya Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu kuhusu namna utawala ghasibu wa Israel unavyokiuka haki ya Wapalestina ya kujitawala na kujiainishia hatima na utawala wao.
Katika upigaji kura, nchi 87 ziliunga mkono azimio hilo, 26 zilipinga na nchi 53 hazikupiga kura. Maoni ya ICJ yenye makao yake The Hague, ambayo yanasuluhisha mizozo kati ya nchi, ni ya lazima yatekelezwe, lakini mahakama hiyo haina uwezo wa kuwajibisha nchi kuyatekeleza. Maamuzi yake, hata hivyo, yana ushawishi mkubwa katika uga kimataifa.
Katika taarifa, watia saini walitaka kubadilishwa hatua za Israeli, wakisema bila kujali msimamo wao juu ya azimio la Baraza Kuu, “tunapinga hatua za kutesa Wapalestina ambazo zimechukuliwa na Israel kama jibu kwa ombi la maoni ya ushauri wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki.”
Katika kukabiliana na mpango uliofaulu wa Palestina katika Umoja wa Mataifa, serikali mpya ya Israel ya mrengo mkali wa kulia imezuia dola milioni 39 za mapato ya kodi yanayokusanywa kwa niaba ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina (PA).