Idadi ya waliouawa katika mripuko wa bomu Nigeria yafikia 40

Wafugaji 40 wa kabila la Fulani wamepoteza maisha huku wengine wengi wakijeruhiwa, baada ya bomu kuwaripukia katika kijiji cha Rukubi, katika mpaka wa majimbo ya Nasarawa na Benue, katikati ya Nigeria.

Awali vyombo vya usalama vya Nigeria vilikuwa vimetaja idadi ya waliouawa kuwa ni 27, lakini taarifa zaidi zinasema, wahanga wa shambulio hilo wameongezeka.

Msemaji wa Polisi katika jimbo la Nasarawa, Ramhan Nansel ameziambia duru za habari kuwa, kamandi ya polisi katika eneo hilo imeanzisha uchunguzi kubaini kiini cha mripuko huo, ili kuwafikisha mbele ya sheria wahusika wake.

Kwa upande wake Gavana wa jimbo la Nasarawa, Abdullahi Sule amesema kuwa, vyombo vya dola vinafanya kila viwezalo kuhakikisha kwamba, waliohusika na umwagaji damu huo wanafikiwa na mkono wa sheria.

Amewataka watu wa kabila la Fulani kuwa watulivu, na wajizuie kuchukua hatua yoyote ya ulipizaji kisasi. Amebainisha kuwa, maafisa usalama wametumwa katika eneo hilo ili kuchunguza chanzo cha shambulio hilo la Jumatano.

Haya yanaripotiwa siku chache tu baada ya genge la watu wenye silaha nchini Nigeria kushambulia kijiji kimoja na kuwaua watu wasiopungua 12 katika shambulizi jipya huko kaskazini-magharibi mwa nchi hiyo ya maghariibi mwa Afrika.

Ukosefu wa usalama umeongezeka sana nchini Nigeria hivi sasa, wakati nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika ikikaribia kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwezi Februari mwaka huu 2023.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *