Mbunge wa chama cha Democratic katika Baraza la Wawakilishi la Marekani amepinga matamshi yaliyyotolewa mwakilishi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa aliyedai kuwa vita vya Russia nchini Ukraine ndio chanzo cha uhaba wa chakula nchini Yemen.
Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) lililazimika kupunguza mgao wa watu milioni nane nchini Yemen mapema mwaka huu (2022) kutokana na ukosefu wa fedha; kwa kadiri kwamba nusu ya familia zinazosumbuliwa na njaa zinaweza kupata chakula cha kila siku kwa shida.
Kwa sasa ukosefu wa ufadhili na misaada ya kimataifa unawaweka watu wengine milioni tano katika hatari ya kukumbwa na njaa nchini Yemen.
Kwa msingi huo maafisa wa Umoja wa Mataifa wametangaza kwamba, Yemen inakabiliwa na maafa makubwa ya binadamu, wakati vita na mashambulizi ya Saudi Arabia na washirika wake vikiingia mwaka wake wa nane.
Akijibu madai ya mwakilishi wa Marekani katika umoja wa Mataifa, Linda Thomas-Greenfield, aliyesema kuwa mashambulio ya Russia dhidi ya Ukraine ndiyo sababu ya uhaba wa chakula nchini Yemen, Ilhan Omar ameandika kwenye ukurasa wa mtandao wa Twitter kwamba: “Mgogoro wa binadamu wenye uharibifu mkubwa huko Yemen haukusababishwa na hujuma ya Russia huko Ukraine.”
Omar ameongeza kuwa, uhaba wa chakula nchini Yemen unatokana na vita na mzingiro wa kikatili wa muungano unaoongozwa na Saudi Arabia ambao unaua mamilioni ya Wayemeni wenye njaa na kwamba Marekani inaendelea kuunga mkono.
Mwaka 2015 Saudi Arabia na washirika wake wakisaidiwa na Marekani, nchi kadhaa za Ulaya kama Uingereza na utawala haramu wa Israel, walianzisha mashambulizi ya pande zote dhidi ya taifa la Yemen na hadi sasa maelfu ya raia wasio na hatia wameuawa na mamilioni ya wengine wamelazimishwa kuwa wakimbizi.