Muungano wa Falme za Kiarabu (Imarati) umetiliana saini na utawala dhalimu na pandikizi wa Kizayuni, makubaliano makubwa na pande zote ya kiuchumi, ikiwa ni pamoja na kupunguza ushuru wa bidhaa.
Kwa mujibu wa televisheni ya “Rusia al Yaum,” Abdullah bin Zayed, Waziri wa Mambo ya Nje wa Imarati na Michal Herzog, mke wa rais wa utawala wa Kizayuni wa Israel wametangaza kuwa, hatimaye Tel Aviv na Abu Dhabi zimetiliana saini makubaliano makubwa ya kiuchumi baina yao.
Ripoti hiyo imeongeza kuwa, makubaliano hayo yanajumuisha pia kuondolewa kikamilufu au kupunguzwa ushuru kwa asilimia 96 wa bidhaa zote zinazoingia na kutoka baina ya pande hizo mbili. Vile vile Imarati na utawala katili wa Kizayuni zimekubaliana kuongeza mabadilishano ya biashara ya bidhaa zisizo za mafuta ambapo hivi karibuni, mabadilishano ya bidhaa hizo yameongezeka kwa asilimia 114, baina ya pande hizo mbili.
Tel Aviv na Abu Dhabi zimeongeza ushirikiano wao pia katika sekta za nishati jadidika, teknolojia na sekta nyingine zinazohusiana na usalama wa chakula.
Naye Thani bin Ahmed Al Zeyoudi, waziri wa biashara za kigeni wa Muungano wa Falme za Kiarabu alisema wiki mbili nyuma kwamba, Abu Dhabi na Tel Aviv zimefikia makubaliano makubwa na mapana ya kiuchumi na kudai kuwa mapatano hayo yatasaidia sekta za viwanda na huduma za Imarati.