Imran Khan anusurika kifo baada ya kupigwa risasi ya mguuni

Imran Khan, Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan amenusurika kifo baada ya gari lake kushambuliwa kwa risasi leo na yeye mwenyewe kujeruhiwa baada ya kupigwa risasi ya mguuni.

Ripoti mbalimbali zinasema kuwa, msafara wake ulishambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana mashariki mwa Pakistan.

Imran Khan alikuwa akiongoza mkusanyiko mkubwa kuelekea mji mkuu Islamabad kudai uchaguzi wa mapema. Taarifa zaidi zinasema kuwa, hali yake kiafya siyo ya hatari ingawa amepigwa risasi ya mguuni.

Fawad Chaundhry, waziri wa zamani wa habari wa Pakistan na mpambe wa karibu wa Imran Khan hakuwa tayari kuzungumzia tukio hilo.

Duru mbalimbali za habari zimelitaja tukio hilo kuwa ni jaribio la kutaka kumuua Waziri Mkuu huyo wa zamani wa Pakistan ambaye anajipanga kurejea tena madarakani baada ya chama chake kuonekana kuwa na uungaji mkono mkubwa katika uchaguzi wa Bunge.

Takriban miezi sita iliyopita, Imran Khan aliondolewa kwenye wadhifa wa uwaziri mkuu wa Pakistan baada ya wabunge kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye. Imran Khan, ambaye anataka ufanyike uchaguzi wa mapema, bila shaka atashikilia zaidi takwa lake hilo kutokana na ushindi huo aliopata.

Awamu ya pili ya uchaguzi wa katikati ya muhula kabla ya uchaguzi mkuu wa Pakistan imefanyika ili kutafuta wawakilishi wa viti 11 vya bunge la taifa na vya majimbo katika miji tofauti ikiwemo Peshawar, Karachi na Multan, ambapo wagombea wa chama cha Tehreek-e-Insaf kinachoongozwa na Imran Khan walifanikiwa kushinda viti vinane, vikiwemo sita vya bunge la taifa na kukiweka chama hicho katika nafasi ya juu zaidi kuliko muungano wa vyama viwili vya Wananchi and Muslim League Nawaz.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *