Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema, azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu mgogoro wa Yemen na lugha iliyotumika katika azimio hilo vitakuwa na taathira hasi kwa mwenendo wa amani na kupanua zaidi ufa uliopo baina ya misimamo ya pande mbili zinazopigana.
Saeed Khatibzadeh ameongeza kuwa, inasikitisha kuona azimio hilo limetumia lugha na misamiati iliyochochewa na utashi wa kisiasa na lobi za nchi zinazounda muungano vamizi huku likikinzana na juhudi zinazofanywa hivi sasa za kuanzisha tena mchakato wa kisiasa.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kuwa, tangu vilipoanza vita vya Yemen, mtazamo wa kuupendelea upande mmoja na usioakisi ukweli halisi wa matukio ya Yemen, ambao uliongozwa na waungaji mkono wakuu wa uvamizi dhidi ya ardhi ya Yemen katika Baraza la Usalama, si tu haukusaidia kupunguza mgogoro, bali umekuwa sababu ya kuendelea na kuchukua muda mrefu hali mbaya zaidi ya maafa ya kibinadamu yanayoshuhudiwa katika karne hii.
Khatibzadeh amebainisha kuwa, matokeo ya kupuuza jinai zinazofanywa na muungano vamizi wa kijeshi na kujiweka mbali Baraza la Usalama la UN na jukumu lake halisi katika kipindi chote cha miaka saba ya vita vya kidhalimu dhidi ya Yemen, ni kuongezeka ukiukaji mkubwa na wa kimfumo wa sheria za kimataifa za huduma za kibinadamu, mauaji ya raia, ubomoaji mkubwa wa miundomsingi isiyo ya kijeshi na mzingiro haramu dhidi ya bandari na viwanja vya ndege mbele ya kimya cha jamii ya kimataifa; na kuendelea kwa hali hiyo, kunatatiza na kuzidisha ugumu wa kupatikana amani endelevu na ya kiuadilifu nchini Yemen.
Siku ya Jumatatu, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliafiki kuendelezwa marufuku ya kuuziwa silaha harakati ya Ansarullah ya Yemen sambamba na kupitisha rasimu ya azimio lililopendekezwa na Imarati linalotaka marufuku ya silaha waliyowekewa baadhi ya viongozi wa Ansarullah ijumuishe pia harakati yote hiyo ya muqawama ya wananchi wa Yemen…/