Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian amesema Jamhuri ya Kiislamu imezifahamisha nchi za Magharibi kuwa katu haitavuka mistari yake miekundu katika mazungumzo ya Vienna ambayo yanalenga kuhuisha mapatano ya JCPOA.
Akizungumza mjini Tehran Jumatano akiwa ameandamana na waziri mwenzake wa mambo ya nje wa Oman Sayyid Badr al-Busaidi, Amir-Abdollahian amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katu haitavuka mistari yake miekundu katika mazungumzo ya Vienna. Amesisitiza kuwa, mazungumzo yanapaswa kuwa yenye manufaa na yenye faida kwa taifa adhimu la Iran.
Amir-Abdollahian amesema mazungumzo katika mji mkuu wa Austria, Vienna yamefika kipindi muhimu sana na kuongeza kuwa, kumebakia masuala machache lakini muhimu sana ambayo yanapaswa kutatuliwa.
Ameongeza kuwa, mjini Vienna, Iran imekuwa ikifanya mazungumzo na wawakilishi wa nchi za 4+1 ambazo ni Russia, China, Ufaransa, Uingereza na Ujerumani. Aidha amesema katika mazungumzo hayo Iran imekuwa ikiwasiliana kwa njia isiyo ya moja kwa moja na Marekani kupitia Enrique Mora, naibu mkuu wa sera za kigeni katika Umoja wa Ulaya. Amesema Marekani imetuma maombi mengi ikitaka mazungumzo ya moja kwa moja na Iran lakini kilicho muhimu ni manufaa ya mazungumzo kama hayo kwani hadi sasa Marekani haijachukua hatua za kivitendo kuonyesha nia njema.
Marekani ilijiondoa katika mapatano ya JCPOA mwaka 2018 na baada ya hapo ikaanza kampeni ya kile ilichokitaja kuwa ni mashinikizo ya juu kabisa na vikwazo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Mazungumzo ya Vienna yanafanyika kwa lengo la kuondoa vikwazo hivyo vya kidhalimu dhidi ya Iran.
Kwingineko Amir-Abdollahian amesema uhusiano wa Iran na Oman ni mzuri na ameutaja kuwa wa aina yake na wa kistratijia katika eneo la Ghuba ya Uajemi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman kwa upande wake amesisitiza kuhusu umuhimu wa uhusiano wa kisiasa baina ya nchi hizi mbili ambao ameutaja kuwa uliojengeka katika msingi wa kuaminiana na kuheshimiana na halikadhalika maslahi ya pamoja.