Iran: Israel inapaswa kuharibu silaha zake za nyuklia na ijiunge na NPT

Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa ameutaka utawala wa Kizayuni wa Israel uharibu silaha zake za nyuklia na ujiunge haraka na Mkataba za Kuzuia Uzalishaji na Usambazaji wa Silaha za Nyuklia (NPT).

Majid Takht Ravanchi alisema hayo katika Mkutano wa Kumi wa Kuangalia Upya Maazimio ya Nchi Wanachama wa Mkataba wa NPT uliofanyika katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York.

Ameeleza wasiwasi wake wa kutotekelezwa azimio la NPT la mwaka 1995, na mpango uliopasishwa mwaka 2010 wa kuhakikisha kuwa eneo la Asia Magharibi unakuwa salama kutokana na silaha za nyuklia.

Amesema utawala wa Kizayuni wa Israel ambao unaungwa mkono na kukingiwa kifua na Marekani unapaswa kujiunga na Mkataba wa Kuzuia Uzalishaji na Usambazaji wa Silaha za Atomiki NPT na uheshimu sheria za kimataifa.

Takh Ravanchi amesema kitendo cha jamii ya kimataifa cha kufumbia macho silaha za nyuklia zinazomilikiwa na utawala dhalimu wa Israel ni hatari kwa usalama wa dunia nzima.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza bayana kuwa, jamii ya kimataifa ina wajibu wa kuilazimisha Israel ijiunge haraka na mkataba wa NPT tena bila ya masharti yoyote.

Ifahamike kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel ndio utawala pekee ambao si mwanachama wa NPT katika eneo la Asia Magharibi licha ya kujilimbikizia silaha hatari za mauaji ya halaiki ya watu.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *