Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema utawala wa Kizayuni wa Israel ndio chimbuko la vitendo vya kigaidi na ukosefu wa usalama na uthabiti katika eneo hili la Asia Magharibi.
Naser Kan’ani alisema hayo jana Jumanne na kuongeza kuwa, hatua ya Marekani kuukingia kifua na kuunga mkono utawala haramu wa Israel inadhihirisha wazi kuwa Washington inaongopa ikidai kuwa inafuatilia amani na usalama katika eneo.
Akijibu madai ya Rais Joe Biden dhidi ya Iran yaliyochapishwa kwenye safu ya tahariri ya gazeti la Washington Post, Kan’ani amesema kitendo cha Biden kung’ang’ania sera iliyofeli ya mtangulizi wake Donald Trump ya mashinikizo ya juu dhidi ya Iran, kinakwenda kinyume na madai ya rais huyo wa Marekani kuwa anataka kuhuisha makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amemuasa Biden atazame mambo kwa uhalisia wake, na awache kujaribu kuzitwisha nchi za eneo hili thamani na sera za Marekani. Amesisitiza kuwa, nchi za eneo zina uwezo wa kusimamia mambo yao na kuamua mustakabali wao.
Kadhalika Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Iran inapinga vikali njama za maadui za kutaka kuundwa eti NATO ya Asia Magharibi, akisisitiza kuwa mpango huo unafanyika kwa maslahi ya utawala wa Kizayuni.
Kwa mujibu wa maafisa wa Baraza la Usalama wa Taifa la Marekani, Biden katika safari yake ya Saudia na katika ardhi za Palestina zilizopachikwa jina la Israel itakayofanyika baina ya leo Julai 13 na 16, atajadili na wenyeji wake juu ya kile kinachodai kuwa ’tishio la Iran’ na vilevile mikakati ya kuiwezesha Israel kupanua satua yake katika eneo.