Iran imesema mauaji ya hivi karibuni ya polisi wa Marekani dhidi ya mwalimu mwenye asili ya Afrika ambaye hakuwa na silaha yanadhihirisha hali mbaya ya haki za binadamu ambayo watu wasio wazungu wanakabiliwa nayo kote Marekani.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Nasser Kan’ani, aliyasema hayo katika ukurasa wake wa Twitter Jumanne, akizungumzia kifo cha, Keenan Anderson, baada ya kushambuliwa na polisi huko Los Angeles, jambo ambalo limezua kilio kikubwa kote nchini humo.
Anderson, 31, binamu wa Patrisse Cullors, mwanzilishi mwenza wa vuguvugu la Black Lives Matter la kutete watu weusi, alifariki katika hospitali ya Santa Monica, California, baada ya kupatwa na mshtuko wa moyo kufuatia kisa cha alasiri ya Januari 3 katika kitongoji cha Los Angeles’ Venice.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameelezea kifo cha Anderson kuwa “cha kusikitisha.” Amekumbusha kwamba mauaji hayo yameambatana na siku ambayo inaadhimisha kuzaliwa kwa Martin Luther King Jr., kiongozi mashuhuri wa haki za kiraia wa Marekani, ambaye alijitolea maisha yake katika kupigania kutendewa haki jamii ya Wamarekani wenye asili ya Kiafrika.
Mauaji hayo, msemaji huyo amesema, yameonyesha kwamba “licha ya kupita miongo mitano kufuatia mauaji ya Luther King, ndoto zake za kutendewa haki Wamarekani Weusi hazijatimia.”
“Watu wa rangi (wasio wazungu),” ameongeza, “bado wako chini ya ukiukwaji mkubwa wa haki za msingi za binadamu na wanaendelea kubaguliwa.”
Idara ya Polisi ya Los Angeles (LAPD) imetoa video za tukio la Januari 3 ambayo inaonyesha Anderson akiomba msaada huku maafisa wakiwa wanamkandamiza
Kwa mujibu wa ripoti, mwalimu huyo wa shule alizomewa mara kwa mara na maafisa wa polisi wa Los Angeles ambao walitumia nguvu ziada dhidi yake kwa sababu ya kosa la sheria za usafiri wa barabarani. Katika picha ya dakika 13 ya kamera ya mwili iliyotolewa na Idara ya Polisi ya Los Angeles, Anderson alionekana akiomba msaada huku maafisa kadhaa wakimshikilia chini na afisa mmoja akiwa ameweka mkono wake kwenye shingo lake.
“Wanajaribu kunifanyia George Floyd,” Anderson alisikika akisema katika video hiyo, akimaanisha mauaji ya polisi wa Marekani dhidi ya Floyd Mei 2020 huko Minneapolis ambayo yalisababisha maandamano makubwa duniani.