Iran: Mpango wa kijeshi wa nyuklia wa Israel ni tishio kwa usalama wa dunia

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema ustawi wa mpango wa kijeshi wa nyuklia wa utawala wa Kizayuni wa Israel na kuendelea kukataa utawala huo vituo vyake vya nyuklia vikaguliwe na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) ni tishio kubwa kwa usalama wa kimataifa.

Nasser Kan’ani Chafi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran aliandika Ijumaa katika ukurasa wake wa Twitter kuwa,’kuendelea mpango wa kijeshi wa atomiki wa utawala wa apathaidi wa Israel na kuendelea utawala huo kukataa kujiunga na Mkataba wa Kimataifa wa Kuzuia Usambazwaji wa Silaha za Nyuklia ni tishio kwa usalama wa kimataifa na mchakato wa kuzuia uenezwaji silaha za nyuklia.”

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameashiria kuteuliwa Mohsen Naziri Asl kuwa mwakilishi wa kudumu wa Iran katika mashirika ya kimataifa huko Vienna Austria na pia katika Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki umefanyika sambamba na maadhimisho ya kuasisiwa IAEA Juni 29 mwaka 1957.

Akimpongeza mwanadiplomasia huyo kwa uteuzi huo amesema inatarajiwa kuwa, Mkurugenzi Mkuu wa IAEA atatekeleza majukumu yake ya kuhimiza utumizi wa nishati ya nyukjia kwa malengo ya amani bila ubaguzi.

Utawala wa Kizayuni wa Israel ambao umekataa katakata kuruhusu wakaguzi wa IAEA kufanya uchunguzi na ukaguzi katika vituo na viwanda vyake vya nyuklia umekataa kutia saini mkataba wa kuzuia usambazaji wa silaha za nyuklia NPT, ambapo unakisiwa kujirundikia vichwa vya nyuklia kati ya 200 hadi 400 katika maghala yake ya silaha za mauaji ya umati.

Silaha hizo zimeundwa kwa kutumia mada ya plutonium ambayo imepatikana katika tanuri nyuklia ya maji mazito ya Dimona. Kituo cha Dimona kinaaminika kuwa muhimu kwa mradi wa Israel wa kuunda silaha za nyuklia.

Utawala haramu wa Israel umepuuzilia mbali miito ya kuweka wazi vituo vyake vya nyuklia ili vikaguliwe na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki. Ukaidi huo wa Israel unatokana na uungaji mkono wa Marekani.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *