Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Guinea zimeazimia kuimarisha zaidi uhusiano wa pande mbili katika sekta ya kilimio ikiwa ni katika mkakati wa Iran wa kuendelea kuboresha zaidi ushirikiano na nchi za Afrika.
Hayo yamebainika katika kikao cha Naibu Waziri Mashauri ya Kigeni wa Iran anayeshughulikia masuala ya kiuchumi na Waziri wa Kilimo wa Guinea Conakry.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Iran Press, Mehdi Safari, Naibu Waziri wa Uchumi wa Mambo ya Nje wa Iran amekutana na Mamadou Nagnalen Barry, Waziri wa Kilimo na Mifugo ya Guinea, na kujadili kupanuka kwa ushirikiano wa pande mbili katika kilimo.
Katika mkutano huo uliofanyika Conakry, huku akirejelea uwezo wa juu wa Iran, hasa katika sekta ya kiviwanda na utafiti katika masuala ya kilimo, Safari ameelezea matumaini yake kwamba, ukuaji wa uhusiano wa pande mbili katika kilimo utaimarishwa kwa kupitia kuhuishwa kamisheni ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.
Mamadou Nagnalen Barry, Waziri wa Kilimo wa Guinea naye ameashiria uhusiano wa zamani kati ya pande hizo mbili tangu uhuru wa Guinea na akaongeza kuwa, maendeleo ya Iran katika nyanja mbalimbali za sayansi na hasa katika kilimo ni ya kuvutia. Ametaka uwezo huo wa Iran utumike katika kuimarisha uhusiano wa nchi hizi mbili rafiki.