Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Anayehusika na Diplomasia ya Uchumi amekutana na kuzungumza kwa nyakati tofauti na Rais na Waziri Mkuu wa Uganda kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa kiuchumi kati ya nchi mbili.
Mahdi Safari amekutana na Waziri Mkuu wa Uganda Robinah Nabbanja na kujadili kuendeleza ushirikiano kati ya nchi mbili khususan katika nyanja za uchumi. Pande mbili hizo aidha zimebadilishana mawazo huku zikifikia makubaliano kadhaa kuhusu kuondoa vizuizi katika kuingiza dawa na zana za kitiba za Iran nchini Uganda.
Itafahamika kuwa, kundi la watafiti wa Kiirani kuhusu mifugo lilitumwa kwa ajili ya kutoa chanjo za wanyama, teknolojia ya kibayolojia, teknolojia ya nano, na kuhusu ushirikiano wa masuala ya teknolojia ya habari, maendeleo ya kilimo na kusambaza vifaa vya kemikali vinavyohitajika huko Uganda.
Akiwa ziarani Kampala mji mkuu wa Uganda, jana jioni Mahdi Safari Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Anayehusika na Diplomasia ya Uchumi amekutana na kuzungumza na Rais Yoweri Kaguta Museveni wa nchi hiyo katika Ikulu ya Entebbe.
Rais Museveni ametuma salamu zake kwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatollah Ali Khamenei na kuashiria safari zake nne za miaka iliyopita hapa Iran na kueleza kuwa tayari alishakuwa mwenyeji wa marais watatu wa Iran na kwamba hivi sasa pia yupo tayari kumkaribisha nchini Uganda Rais Ebrahim Raisi.
Mahdi Safari na Yoweri Museveni aidha wamesisitiza kupanua ushirikiano wa kiuchumi, kisiasa na wa kimataifa kati ya nchi mbili sambamba na kuwa na tume ya pamoja ya ushirikiano, kutuma madawa, zana za kitiba, bidhaa za nano na zile zinazozalishwa kwa kustafidi na bio-teknolojia, masuala ya habari, ushirikiano wa kibenki, kutuma nchini Uganda kundi la wataalamu watafiti wa tiba kutoka Iran ili kuona namna nchi mbili zinavyoweza kushirikiana katika kutoa tiba kwa maradhi mbalimbali ya mifugo na masuala mengineyo.