Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema kuwa na uwezo wa kujirushia satalaiti katika anga za mbali ni kigezo cha nchi iliyostawi duniani na kuongeza kuwa, pamoja na kuwepo vikwazo vingi vya kimataifa, vijana wa taifa la Iran katika IRGC wamefanikiwa kurusha satalaiti katika anga za mbali.
Jana Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu lilitangaza limerusha kwa mafanikio makubwa satalaiti iliyopewa jina la Nour-2 ya kijeshi ya Iran katika anga za mbali.
Kwa mujibu wa taarifa satalaiti hiyo imerushwa katika anga za mbali katika umbali wa zaidi ya kilomita 500 kutoka ardhini.
Huko nyuma yaani mwaka 2020 Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) limewahi kurusha satalaiti ya Nour-1 iliyokuwa satalaiti ya kwanza ya kijeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ambayo ilirushwa umbali wa kilomita 425 kutoka ardhini.
Baada ya kurushwa kwa mafanikio satalaiti ya Nour-2, sasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina satalaiti mbili za kijeshi katikka anga za mbali ambapo moja iko umbali wa kilomita 425 na nyingine umbali wa kilomita 500 kutoka ardhini.