Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amelaani shambulio la utawala ghasibu wa Israel katika mji wa Nablus katika Ukingo wa Magharibi huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu, na kuutaja uungaji mkono usio na kikomo wa Marekani na nchi nyingine za Magharibi kwa utawala dhalimu wa Israel kuwa ni kielelezo kikubwa zaidi cha ukiukwaji wa haki za binadamu.
Wapalestina sita waliuawa shahidi na wengine wasiopungua 22 kujeruhiwa katika shambulio la jana asubuhi la utawala wa Kizayuni kwenye miji ya Nablus na Ramallah katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran, Nasser Kan’ani, ameashiria jinai na vitendo vya kigaidi vinavyoendelea kufanywa na Wazayuni huko Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ikiwa ni pamoja na kuzingirwa na mashambulizi dhidi ya eneo la Nablus, na ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua ya kukomesha na kulaani mauaji ya halaiki yanayofanywa na Wazayuni huko Palestina.
Kan’ani amepongeza mapambano na ushujaa wa Wapalestina hususan vijana wa Baitul Muqaddas na ameyahimiza mataifa na nchi mbalimbali kuunga mkono mapambano ya kupigania uhuru ya watu wa Palestina.
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran aidha amekosoa misimamo ya kinafiki na kindumakuwili ya Marekani na baadhi ya nchi za Magharibi kuhusiana na masuala ya haki za binadamu na kusema: Uungaji mkono wao usio na masharti kwa utawala ghasibu wa Israel na jinai za kila siku za utawala huo haramu dhidi ya taifa madhulumu la Palestina ni mfano mkubwa zaidi wa ukiukaji wa haki za binadamu ambao unaendelea kwa miongo mingi.