Iran yaikashifu WSJ ya U.S kwa kuchapisha makala yasiyoridhisha

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelikosoa vikali gazeti la Kimarekani la Wall Street Journal kwa kuchapisha makala ya kipumbavu na ya kihasama dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, wakati huu wa kuendelea kufanyika mazungumzo ya kuiondolea vikwazo Iran huko Vienna.

Taarifa ya Ubalozi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa imesema kuwa, hatua ya gazeti hilo ya kushajiisha na kuchochea moto wa kushambuliwa kijeshi vituo vya nyuklia vya Iran inakanyaga waziwazi kanuni na sheria za kimataifa.

Taarifa hiyo imetahadharisha kuwa, wapangaji na watekelezaji wa njama hizo chafu dhidi ya vituo vya kiraia vya Iran watabeba dhima ya matokeo mabaya ya chokochoko hizo.

Katika tahariri iliyochapishwa juzi Januari 6, gazeti hilo la Kimarekani la WSJ lilimtaka Rais Joe Biden wa Marekani ajiandae kwa ajili ya kuvishambulia kijeshi vituo vya kuzalisha nishati ya nyuklia vya Iran, iwapo mazungumzo hayo ya Vienna yatagonga mwamba.

Duru ya nane ya mazungumzo ya Vienna, ambayo ajenda yake kuu ni kuondolewa vikwazo vya kidhalimu na visivyo vya kisheria ilivyowekewa Iran, ilianza mwishoni mwa mwaka uliomalizika.

Marekani ambayo ilijiondoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA mnamo Mei mwaka 2018 na kusababisha mkwamo kwenye utekelezaji wa mapatano hayo, inashiriki mazungumzo ya Vienna nchini Austria kwa njia isiyo ya moja kwa moja.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *