Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ametuma salamu za rambirambi kwa serikali na wananchi wa Tanzania kufuatia ajali ya ndege iliyosababisha vifo vya raia kadhaa wa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Nasser Kan’ani amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesikitishwa na kuhuzunishwa na vifo vya watu 19 walioaga dunia kufuatia kuanguka ndege ya abiria ya Tanzania na kutoa mkono wa pole kwa serikali na watu wa nchi rafiki ya Tanzania.
Watu 19 wakiwemo abiria 17 pamoja na rubani na msaidizi wake waliaga dunia na wengine zaidi ya 20 walijeruhiwa katika ajali ya ndege ya Shirika la Precision Air iliyotokea Jumapili asubuhi wakati ndege hiyo ilipoanguka katika Ziwa Victoria jirani kabisa na uwanja wa ndege wa Bukoba.
Ndege hiyo ilikuwa na watu 43, kati yao 39 wakiwa abiria, marubani wawili na wahudumu wawili.
Kwa mujibu wa taarifa, ndege hiyo ya Precision Air namba PW494 iliyokuwa ikitoka Dar es Salaam kwenda Mwanza kupitia Bukoba, ilianguka katika Ziwa Victoria muda mfupi kabla ya kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Bukoba.
Abiria 28 wameokolewa katika ajali hiyo.
Kufuatia ajali hiyo ya ndege, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alitoa salamu za pole akisema: “nimepokea kwa masikitiko taarifa ya ajali ya ndege ya Shirika la Precision katika Ziwa Victoria, mkoani Kagera. Natuma salamu za pole kwa wote walioathirika na ajali hii”.