Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amelikosoa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kusisitiza kuwa: Mwelekeo wa sasa na usio na tija wa Baraza la Usalama la Uumoja huo unaupa moyo na kuuhamasisha utawala wa Kizayuni katika kadhia ya Palestina.
Amir Saeed Iravani amesema katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba: “Leo hii wananchi wa Palestina wanahitajia himaya na hatua madhubuti za Baraza la Usalama ili kuweza kukomesha hujuma na uvamizi wa utawala ghasibu wa Israel, na kutoa matamshi ya kueleza masikitiko na mshikamano na watu wa Palestina peke yake hakutoshi.”
Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Iran katika UN ameongeza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu inaona kuwa ni wajibu wake kuunga mkono haki halali za Palestina kwa ajili ya kukabiliana na ukandamizaji na uchokozi wa utawala huo wa kibaguzi na inauona kuwa ni katika muelekeo wa kuwapa Wapalestina haki ya kujiamulia mustakbali wao. Amesisitiza kuwa hiyo ni miongoni mwa sera za kimsingi za Iran hadi pale uvamizi wa Israel huko Palestina utakapokomeshwa.
Iravani amesema kuwa, hali inayotawala ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu imekuwa mbaya zaidi.
Balozi wa Iran UN ameongeza kuwa: Utawala wa Kizayuni unaendeleza mienendo yake ya kibaguzi ikiwa ni pamoja na kujitanua, ukandamizaji, ukiukaji wa haki za binadamu za Wapalestina kupitia mauaji ya watu wasio na hatia wakiwemo wanawake na watoto, kuiba na kuharibu mali ya Wapalestina na kuwafukuza kwa mabavu katika makazi na nyumba zao.
Iravani amesema kuwa: Leo hii, Gaza imekuwa jela kubwa zaidi duniani, na watu wengi wakiwemo wanawake na watoto, wanasumbuliwa na vikwazo na ukiukwaji wa haki za kimsingi, mambo ambayo ni uhalifu dhidi ya ubinadamu, ukiukaji wa sheria zote za kimataifa na ni tishio kubwa kwa amani na usalama wa kimataifa.