Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran mapema leo alfajiri amelaani shambulio la kigaidi lililotokea jana jioni mjini Istanbul Uturuki na kuua na kujeruhi makumi ya watu.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Nasser Kan’ani amesema, Tehran inalaani kitendo chochote cha kigaidi ambacho kinahatarisha usalama wa nchi na wananchi wa Uturuki.
Vile vile amewaombea dua na msamaha wa Mwenyezi Mungu wote waliouawa kwenye shambulio hilo la kigaidi kama ambavyo amewaombea pia afueni ya haraka majeruhi. Pia amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatoa mkono wa pole kwa serikali, kwa wananchi wa Uturuki na familia za wahanga wa shambulio hilo.
Jana jioni watu 6 waliuawa na wengine 81 walijeruhiwa baada ya kutokea shambulio la kigaidi katika eneo lenye watu wengi la Taksim mjini Istanbul.
Usiku wa kuamkia leo, Makamu wa Rais wa Uturuki, Fuat Oktay amesema kuwa, mwanamke ndiye aliyefanya shambulio hilo la kigaidi kwa kujiripua kwa mabomu kwenye eneo hilo lenye watu wengi.
Kabla ya hapo, Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki naye alikuwa amesema, nchi yake haitotetereshwa na vitendo kama hivyo vya kigaidi.
Aidha alisema katika hotuba yake hiyo ya jana usiku kwamba, tathmini za awali zinaonesha kuwa shambulio hilo ni la kigaidi.