Iran yamtia mbaroni kinara wa chombo cha kigaidi cha ‘Iran International’

Vyombo vya usalama vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vimemtia mbaroni kinara wa chombo cha habari cha kigaidi kinachojiita ‘Iran International’ huko kaskazini magharibi mwa nchi.

Taarifa ya Kituo cha Kijeshi cha Hamzah Sayyidu Shuhadaa imeeleza kuwa, kiongozi huyo wa ‘Iran International’ amekamatwa baada ya kufuatiliwa na kutambuliwa na vikosi vya usalama vya Jamhuri ya Kiislamu ambavyo viko macho.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, kiongozi huyo wa shirika hilo la habari linalofadhiliwa na Saudi Arabia amekamatwa na maafisa usalama katika mji wa Khoy, mkoani Azarbaijan Magharibi, kaskazini magharibi mwa Iran.

Taarifa hiyo imebainisha kuwa: Kufuatia ghasia za hivi karibuni katika mji huo (Khoy), ajenti mkuu wa kanali ya Kisaudia ya Iran International amekamatwa katika operesheni kabambe vya maafisa usalama.

Kituo cha Kijeshi cha Hamzah Sayyidu Shuhadaa cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) kimeongeza kuwa, wakala huyo wa ‘Iran International’ aliyekamatwa, alikuwa anawachochea wananchi wachukue hatua za kuhujumu usalama wa taifa la Iran.

Haya yanajiri siku chache baada ya Kamanda wa Kikosi cha Nchi Kavu cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu kutangaza habari ya kutumwa wanajeshi zaidi katika mipaka ya magharibi na kaskazini magharibi mwa Iran ili kupiga jeki operesheni za kukabiliana na makundi ya kigaidi yanayotaka kujitenga na yanayochoche fujo hapa nchini.

Wizara ya Intelijensia ya Iran hivi karibuni iliitambua kanali ya Iran International inayofadhiliwa kwa hali na mali na serikali ya Riyadh kuwa shirika la kigaidi.

 

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *