Iran yapongeza misimamo ya Namibia ya kuliunga mkono taifa la Palestina

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu amesifu misimamo ya Namibia ya kuliunga mkono taifa la Palestina na kusisitizia malengo ya pamoja ya Tehran na Windhoek.

Hussein Amir-Abdollahian amesema hayo katika mazunguumzo yake kwa njia ya simu na Bi Netumbo Nandi-Ndaitwah, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Namibia na kueleza matumaini yake ya kuongezwa ushirikiano wa Iran na Namibia katika nyuga mbalimbali.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amebainisha kwamba, Tehran inasifu na kupongeza misimamo ya Namibia kuhusiana na kadhia ya Palestina ambayo imekuwa ikipewa kipaumbele pia na Tehran.

Kuhusiana na uhusiano wa pande mbili, Abdollahian ameeleza kwamba, uhusiano wa Iran na Namibia ni mzuri na umo katika hatua ya kustawi zaidi na kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inakaribisha kwa mikono miwili hatua za kupanua zaidi ushirikiano baina ya pande mbili hasa katika nyuga za kielimu, teknolojia na kilimo.

Kwa upande Bi Netumbo Nandi-Ndaitwah, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Namibia ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu wa nchi hiyo ameashiria katika mazungumzo yake hayo ya simu juu ya himaya na uungaji mkono wa Iran kwa Namibia katika kipindi cha kupigania uhuru na kueleza kwamba, taifa lake linakaribisha hatua za kuweko ushirikiano zaidi baina ya pande mbili katika nyuga mbaliimbali.

Amesema, kuna nyanja nyingi ambazo Iran na Namibia zinaweza kushirikiana na akaeleza kwamba, ana matumaini ya kufanya safari mjiini Tehran muda si mrefu.

Ikumbukwe kuwa, mwaka jana Namibia ilikuwa miongoni mwa mataifa ya Kiafrika yaliyolalamikia vikali kitendo cha kuruhusiwa utawala haramu wa Israel kuwa mwanachama mtazamaji katika Umoja wa Afrika (AU).

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *